MWANANCHI
Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande baada ya kuwepo malalamiko ya ubabaishaji katika zabuni mbalimbali za mamlaka hiyo.
Hatua hiyo ya Sitta imekuja wiki tatu baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuiongoza wizara hiyo akitokea Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla, wizara hiyo ilikuwa chini ya Dk Harrison Mwakyembe.
Sitta, ambaye pia hujulikana kama Mzee wa Viwango, amewaambia waandishi wa habari jijini hapa leo kuwa wadau mbalimbali wamesema taratibu za zabuni TPA haziendeshwi kwa uwazi na uaminifu.
“Wanasema hakuna uwazi katika zabuni, kuna dalili ya ubabaishaji. Katika kamati za kutathmini zabuni majina ya watu yanabadilika badilika na hata baada ya mshindi kupatikana bodi huchelewa kutoa barua inayohusu uamuzi wa kumpata mshindi huyo”:- Sitta.
Kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za bandari, amesema ameamua kumsimamisha Kipande kupisha uchunguzi kwa kipindi hicho na nafasi yake itachukuliwa na Meneja Bandari ya Dar es Salaam, Awadh Massawe.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa kamati ya hesabu za Serikali ‘PAC’ Zitto Kabwe amewataka wamiliki wa malori ya mafuta kutafuta biashara nyingine ya kufanya kabla Serikali haijaachana na usafirishaji huo.
Akitoa maoni yake kabla ya kukagua mitambo ya kupima ujazo wa mafuta yanayopakuliwa kutoka melini ,alisema matumizi ya barabara kusafirisha mafuta hayana tija kwa Serikali.
“Kuna haja ya Serikali kujenga mabomba ya mafuta kuelekea mikoani ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato,tutaishauri Serikali inunue asilimia 50 ya hisa za kampuni ya Tiper ili iiendeshe kwa asilimia 100,wamiliki wa malori ni vyema wakaanza kufikiria biashara nyingine watakayofanya“:-Zitto.
Alisema kama suala hilo litatekelezwa Serikali itanusuru uharibifu wa barabara unaotokana na uzito mkubwa wa malori
NIPASHE
Wakati Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza likiendelea kumsaka mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Pendo Emmanuel (4) kwa siku ya 51 sasa aliyeibwa kijiji cha Ndami, Kwimba na watu wasiofahamika Desemba 27, mwaka jana, mtoto mwingine albino ameibwa mbele ya wazazi wake katika kijiji cha Ilelema, wilayani Chato, Geita.
Mtoto huyo, Yohana Bahati, mwenye umri wa mwaka mmoja, aliibwa usiku wa kuamkia jana, akiwa amebebwa na mama yake, Esther Bahati (30), ambaye alivamiwa na watu hao na kupigwa mapanga akiwa jikoni kisha kuporwa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alisema tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi saa 2:00 usiku, wakati mama huyo akiwa jikoni anapika chakula na watu hao kumvamia na kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Watu wasiofahamika walimjeruhi mama wa mtoto kisha kumtwaa mgongoni pasipo kumdhuru na kutoweka sehemu isiyojulikana mpaka sasa hajapatikana wakati jeshi la polisi likiendelea kuwasaka waliotenda uhalifu huo”:- Konyo.
Konyo alisema Esther baada ya kujeruhiwa kwa mapanga, aliwahishwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa usoni, mikononi na mabegani alipokuwa akijaribu kupambana na watu hao wasimchukue mwanaye.
Alisema kutokana na tukio hilo, polisi mkoani Geita inamshikilia baba wa mtoto huyo, Bahati Misalaba, ambaye wakati tukio hilo linatokea alikuwa akiota moto nje ya nyumba hiyo.
NIPASHE
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Dodoma, Frola Mhele, ameambia Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuwa aliyekuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Pcificus Clerofas Simon, alipelekwa kwake kuungama kumuua aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni Chanel Ten Mkoa wa Iringa, Daud Mwangosi, kwa bomu bila kukusudia.
Mhele aliyasema hayo jana mbele ya Jaji wa Mahakama hiyo, Paulo Kihwelo, wakati akitoa ushahidi wa kesi ya mauaji ya Mwangosi.
Hakimu huyo ambaye ni shahidi wa tatu, alidai kuwa mtuhumiwa huyo alipelekwa kwake kuungama wakati akiwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mjini Iringa.
Alidai Septemba 5, 2012 saa 7:24 mchana, polisi walimpeleka mtuhumiwa huyo katika mahakama hiyo kwa ajili ya ungamo na kuchukua maelezo.
Shahidi huyo alidai alimkagua mtuhumiwa mwilini mwake na kumkuta akiwa na jeraha bichi kwenye mkono wake wa kulia katika kidole cha kati kutoka mwisho na majeraha ya zamani.
Mhele alidai alipomuuliza kuwa jeraha amelipatia wapi, alimjibu alilipata wakati bomu lilipolipuka na kwamba hakujua kama amepata jeraha hilo.
MTANZANIA
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, amesema watu waliopambana na askari polisi na wale wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ni kikundi cha wahuni.
Harakati za mapambano baina ya polisi na wahalifu hao zilidumu kwa takribani saa 48, huku Mkuu wa Mkoa huo, Said Magalula akikiri kwamba wameshindwa kuwakamata watu hao.
Jana Ndaki aliwaambia waandishi wa habari kuwa, jeshi hilo linawashikilia watu kadhaa kutokana na tukio la majambazi kushambiliana na askari polisi usiku wa kuamkia Jumamosi.
“Kuna watu kadhaa tumewakamata kuhusika na tukio hilo na upelelezi zaidi unaendelea ili kuweza kuwakamata wote waliohusika.
“Niwatoe hofu wananchi, tukio zima lilihusisha kikundi kidogo cha wahuni ambacho walikuwa wanajificha katika Mapango ya Kijiji cha Mleni kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuhalifu “ :-Ndaki.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula, alisema hali katika Mji wa Amboni ni salama na kuwa, waliookuwa wanapambana na polisi ni majambazi na si magaidi.
MTANZANIA
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amesema kwa muda wa miaka kadhaa sasa baadhi ya vyama vya siasa wilayani Ludewa vimekuwa vikimshawishi atoke kwenye chama chake jambo ambalo amekuwa akilipinga.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara wa sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kijiji cha Nsele, Kata ya Kilondo wilayani hapa, alisema hata mapokezi aliyoyapata yalikuwa ya vyama vyote, vikiwamo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), huku baadhi yao wakimshawishi ahamie kwenye vyama vyao.
Filikunjombe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema wapinzani wanamthamini na kuona kazi zake akiwa CCM, hivyo ataendelea kuwajibika kwa wananchi akiwa ndani ya chama hicho.
“Nimekuja hapa nimepokewa na vijana na viongozi wa vyama vyote, hasa vya Chadema, CUF na TLP, na wengine wakati wananibeba walidiriki kuniambia kuwa wana hofu nitakatwa jina kwenye chama changu na kama itakuwa hivyo nijiunge na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),:- Filikunjombe.
Akizungumzia maendeleo ya Kata ya Kilondo, mbunge huyo alisema awali ilikuwa haina huduma za maendeleo ambapo Januari 30, mwaka huu alikwenda na wahandisi wa umeme na kuzindua mradi wa umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya wilayani humo.
Lakini kutokana na kasi ya utekelezaji wa mradi huo vijiji vyote vya Kata ya Kilondo kabla ya kufikia Desemba mwaka huu vitakuwa vimepata huduma ya umeme ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma za maendeleo.
HABARILEO
Mwanafunzi wa Darasa la Saba, Adam Abdul Sapi (13) ametawazwa kuwa Chifu mpya wa Wahehe, akirithi nafasi ya baba yake, aliyefariki na kuzikwa jana mkoani Iringa.
Rais Jakaya Kikwete alishiriki jana maziko ya Chifu huyo wa Wahehe, Abdul Sapi Mkwawa (66) yaliyokwenda sanjari na hafla ya kumsimika mtoto huyo kushika wadhifa huo wa kimila.
Maziko ya kiongozi huyo aliyefariki Februari 14, mwaka huu, yalifanyika katika kijiji cha Kalenga, nje kidogo ya mji wa Iringa ndani ya makumbusho yaliyowekwa fuvu la babu yake,Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga Mkwawa.
Mbali na Rais Kikwete, wengine waliohudhuria maziko hayo ambayo taratibu zake zilitumia takribani saa 2.30 kuanzia saa 7 mchana ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Tanzania Bara, Phillip Mangulla, wakuu wa mikoa ya Iringa na Mbeya na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa.
Kabla ya kifo chake kilichosababishwa na maradhi ya sukari na figo, Abdul Sapi Mkwawa aliyekuwa mtoto wa tatu wa Spika wa kwanza mweusi nchini, Adam Sapi Mkwawa, alikuwa akifanyakazi katika kiwanda cha maji Afrika cha Kidamali, Iringa.
HABARILEO
Kampuni ya Acacia inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Buzwagi mkoani Shinyanga, imesema ndani ya miaka miwili, itasitisha shughuli za uchimbaji na uzalishaji madini hayo, kutokana na soko kuzidi kushuka.
Meneja Mkuu wa mgodi huo, Filbert Rweyemamu alisema hayo juzi katika kikao cha pamoja baina ya mgodi na wajumbe wa Kamati ya Kijiji cha Mwime, iliyoundwa na uongozi wa mtaa wa Mwime kwa ajili ya kusainiana mkataba wa shughuli za maendeleo.
Rweyemamu alisema shughuli za uzalishaji na uendeshaji ni tofauti na mauzo, hivyo kampuni inazidi kutumia gharama kubwa za uendeshaji.
“Kutokana na mgodi kusitisha shughuli za uzalishaji ndani ya miaka miwili ijayo; siyo kwamba dhahabu zimeisha dhahabu ni nyingi mno, isipokuwa tunashindwa kumudu gharama za uzalishaji wilaya ya Kahama ina dhahabu tangu hatujaingia, makampuni mengi yalichimba na kuondoka na sisi tunaondoka”, alisema meneja huyo.
Bei ya dhahabu kwa mwaka 2014, imekuwa chini ya dola 1,300 kwa ounce moja kwa muda mrefu. Kufikia Novemba, bei ilikuwa 1,129 kwa ounce moja, hali ambayo imeleta mtikisiko wa uendeshaji wa kampuni za uchimbaji wa dhahabu.
Baada ya kujadili upya, walibaini baadhi ya miradi ya vyoo vitano vinavyogharimu Sh milioni 51 na visima vitano vinavyogharimu Sh milioni 140, havikuwemo katika rasimu hiyo, hali iliyopingwa na Meneja wa mgodi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook