MWANANCHI
Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeziagiza kampuni za simu kutoa maelezo kuhusu mabadiliko ya gharama za vifurushi vya muda wa maongezi, Vodacom Tanzania imeeleza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na ongezeko la kodi na hivyo kulazimika “kubadili mazingira ya kibiashara ili kuepuka hasara”.
Kampuni nyingine kubwa ya mawasiliano, imeahidi kutoa ufafanuzi wa suala hilo kesho wakati Airtel imesema haijafanya mabadiliko yoyote kwenye gharama za vifurushi vyake.
Kumekuwapo na mijadala mingi katika mitandao ya kijamii kupinga bei mpya za vifurushi hivyo ambazo zimeelezwa kuwa ni megabati nane kwa vifurushi vyote vya saa 24, na megabati 60 kwa vifurushi vya wiki.
Bei hizo zinaelezwa kuwa zimeanza kutumika kwa wateja wanaotumia mitandao mbalimbali ya simu ambayo inachuana sokoni, huku baadhi ya wateja wa kampuni ambazo hazifanya mabadiliko ya gharama hizo wakiwashiwishi wenzao kuhama ili kutokuwa hewani kutokana na kukosa vifurushi.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Prof. John Nkoma alisema kuwa tayari mazungumzo kati ya mamlaka yake na kampuni hizo za mawasiliano yameshafanyika na kilichobaki ni wao kutoa maelezo ya hatua walizoichukua.
“Matumizi ya intaneti yameongezeka nchini na wananchi wengi wamekuwa hawajui namna ya kutofautisha vifurushi vya muda wa maongezi na vile vya intaneti. Lakini nimezungumza na kampuni zote na tumefikia mwafaka. Ndani ya wiki hii watatoa tamko lao pamoja na msimamo wa bei za vifurushi,”:-Nkoma.
MWANANCHI
Mama wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ambaye alitekwa juzi na watu wasiofahamika mkoani Geita, amefanyiwa upasuaji wa kichwa na jopo la madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando mjini Mwanza.
Mama huyo aliyefahamika kwa jina la Ester Jonas (30), alilazimika kufanyiwa upasuaji huo baada ya kushambuliwa kwa kukatwa mapanga na watu hao ambao walimteka mtoto wake juzi akiwa amembeba mgongoni nyumbani kwake.
Mkuu wa Kitengo cha dharura cha Hospitali ya Bugando, Dk Darick David alisema mama huyo alifikishwa hapo jana akiwa na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Namkumbuka mwanangu Yohana Bahati,” hayo ni maneno aliyoyasema mama mzazi wa mtoto huyo akiwa hospitalini hapa kwenye chumba namba 903 cha uangalizi maalumu (ICU).
“Kama mnavyomuona hali yake siyo nzuri, hata kuzungumza hawezi, alikatwa panga kichwani jeraha kubwa liko puani, tumelazimika kumfanyia upasuaji wa kichwa ili kusafisha damu iliyokuwa imeganda ndani,” alisema Dk David na kuongeza: “Bado anatatizo kubwa na madaktari bingwa wanaendelea kumchunguza.”
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, ProF. Alfred Mteta alisema: “Inasikitisha kuona binadamu unamfanyia unyama binadamu mwenzako, kamwe vitendo hivi haviwezi kukubalika tumempokea mgonjwa huyu na madaktari wanaendelea kumpatia matibabu ili kuokoa maisha yake.”
MWANANCHI
Matukio ya ujambazi na mauaji ya kutumia silaha, yameanza kuibuka kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hali hiyo imekuwa ikihojiwa na wananchi na wapenda amani na zaidi ni kuhusu intelijensia ya polisi kushindwa kugundua mipango ya uhalifu.
Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa kushamiri kwa matukio hayo kunaleta hofu katika jamii huku jamii yenyewe ikilaumiwa kwa kukaa kimya kwa watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na hutumia isivyo halali.
Hali hiyo imetokea mjini Magu, mkoani Mwanza kwa watu wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto usiku wa kuamkia jana walifunga Mtaa wa Kisesa Kata ya Kisesa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza na kumuua mfanyabiashara Nestory Andrew umbali wa mita 50 kilipo Kituo cha Polisi.
Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku, majambazi hayo yalifunga Barabara ya Mwanza-Musoma kwa muda na kusababisha taharuki kwa wakazi wa Kisesa huku milio ya bunduki ikitawala anga.
Wakizungumza na Mwananchi eneo la tukio jana, mashuhuda walisema walianza kusikia milio mizito ya vitu kama bomu na kwamba baada ya muda wakaona watu wakivamia duka la mfanyabiashara huyo na kupiga risasi hewani.
Mmoja ya mashuhuda hao, Daud Mwalimu alisema “Mimi ni fundi baiskeli hapa stendi jana (juzi) muda kama wa saa mbili usiku nilisikia sauti ya vishindo kama bomu, lakini baada ya muda nikasikia sauti za bunduki hewani,”
NIPASHE
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, ‘amefunguka’ kuhusu kashfa inayomkabili ya kupata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwenye fedha zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), akisema hastahili kuitwa mwizi, bali anapaswa kuitwa ‘nyoka wa makengeza’.
Amesema anapaswa kuitwa ‘nyoka wa makengeza’ kwa kuwa yeye ni mjanja wa kutafuta fedha kwa ajili ya wananchi wa jimbo lake, ambao wanapaswa kupuuza madai ya wizi yanayoelekezwa kwake, badala yake wamwamini zaidi.
Chenge, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mstaafu, alisema hayo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mahaha kata ya Bunamala, Wilaya Bariadi mkoani Simiyu juzi.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa kimya, lakini ameshangazwa na kitendo cha kuandamwa kuhusiana na kashfa ya akaunti hiyo.
“Wanasema Chenge na Escrow…Pale nimeenda kutafuta kwa ajili ya wananchi wa jimbo langu wala sikwenda kubomoa duka. Bali tunatumia akili kutafuta pesa kwa ajili yenu,” :- Chenge.
NIPASHE
Siku moja baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kutangaza kumsimamisha kazi kwa muda usiojulikana Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Madeni Kipande, Mkurugenzi huyo ameibuka na kueleza kuwa ameshangazwa na uamuzi huo kwa kuwa hakuwahi kuitwa kabla na Bodi ya Wakurugenzi wa TPA kuelezwa tuhuma hizo kama taratibu na sheria zinavyoelekeza.
Sitta alisema alimsimamisha kazi Kipande kutokana na tuhuma za kukiuka taratibu za zabuni pamoja na mahusiano mabaya na wateja wa mamlaka hiyo.
Kipande alisema tuhuma zilizotolewa kwake siyo za kweli na wala hakuna taratibu zozote za zabuni zilizokiukwa kama ilivyoelezwa na Sitta.
“Sijaitwa na Bodi kuulizwa kabla kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwangu isipokuwa Waziri alikuja jana (juzi) na kusema anataka kikao cha Bodi kuzungumza na wajumbe,” alisema.
Kwa mujibu wa taratibu, Mkurugenzi wa TPA ndiye Katibu wa Bodi, hivyo vikao vyote vya Bodi vinapaswa kuitishwa na yeye kujadili mambo yote yanayohusu TPA.
Kipande alisema kwa kuwa Waziri Sitta ameunda kamati kuchunguza tuhuma zilizoelekezwa kwake, ana imani kuwa kamati hiyo itatenda haki ili ukweli wa mambo aliyotuhumiwa ujulikane.
“Tumekutana katika kikao cha dharura cha Bodi ya Bandari kutokana na kuzingatia malalamiko ya sehemu mbalimbali kwamba taratibu za zabuni TPA hazikukaa sawa, zinaendeshwa katika namna ambayo hazileti imani, nampongeza Dk. Harrison Mwakyembe, alianza vizuri kushughulikia suala hili, lakini bado tatizo halijaisha,” :- Sitta.
NIPASHE
Zaidi ya wanafunzi 3, 000 wa shule nne za msingi za Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba, Mkoa wa Mbeya, wameandamana na kufunga barabara Kuu ya Tunduma – Sumbawanga na ya Tanzania – Zambia na kusababisha shughuli za kiuchumi kusimama kwa zaidi ya saa tano katika mji wa Tunduma.
Katika tukio hilo, wanafunzi hao walimgomea Mkuu wa Wilaya ya Momba, Abiudi Saideya, alipowaomba watawanyike.
Wanafunzi hao kutoka Shule za Msingi Tunduma, Mlimani, Umoja na Mwaka, waliandamana jana kuanzia saa 12:30 alfajiri na kuendelea kukaa barabarani hadi saa 5:40 asubuhi wakiishinikiza serikali kuweka matuta eneo la Mwaka lilikopo barabara kuu ya Tunduma – Sumbawanga jirani na wanakosoma ili kuepusha ajali kuendelea kutokea.
Hatua ya wanafunzi kuandamana ilitokana na ajali ya lori lililokuwa likitokea Sumbawanga kwenda Tunduma kuwagonga watatu na kusababisha wawili kufa na mwingine kujeruhiwa vibaya.
Mmoja alikufa papo hapo na mwingine wakati akipatiwa matibabu Kituo cha Afya cha mjini Tunduma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema mwanafunzi Emmanuel Sichone, alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na lori hilo na Betiel Mbwambwa, alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu kwenye kituo hicho.
Kamanda Msangi alisema mwanafunzi, Jackson Sichone amejeruhiwa vibaya na anaendelea kupatiwa matibabu kituoni hapo.
MTANZANIA
Muuza mishikaki mmoja katika kituo cha daladala cha Temeke mwisho jijini Dar es Salaam maarufu kwa jina la Said Mishikaki, amekamatwa na kupigwa na wananchi kwa tuhuma za kuuza mishikaki ya nyama ya paka.
Said alikamatwa jana asubuhi baada ya taarifa kusambaa katika eneo hilo zikimtuhumu kwamba amekuwa na kawaida kuuza mishikaki ya nyama ya paka badala ya ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine wanaoliwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio zinasema kuwa, baada ya taarifa hizo kuenea, wananchi walilazimika kumtafuta muuza mishikaki huyo ili wamchukulie hatua.
Baada ya kumsaka kwa dakika kadhaa, hatimaye walifanikiwa kumkamata na kumkuta akiwa na paka mmoja aliyekuwa amemchinja na kumuweka kwenye ndoo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wananchi hao walipomuona paka huyo akiwa amechinjwa, walichachamaa na kuanza kumshushia kipigo muuza mishikaki huyo na kumuumiza sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Nilikwenda eneo la tukio na kukuta kielelezo cha mfuko wa nyama hiyo. Niliona nyama na utumbo mkubwa unaoonekana kama ni wa mnyama anayekula majani mfano wa ng’ombe.
“Inawezekana kuna matatizo katika biashara, huenda kweli ile ilikuwa nyama ya paka, lakini hatuna uhakika, hivyo tumechukua vipande vya nyama kwa ajili ya kuvipeleka kwa mtaalamu wa mifugo kwa uchunguzi zaidi ili kubaini aina hiyo ya nyama”Alisema kamanda Kihenya.
HABARILEO
Wakati serikali ikianza kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo wafanyabiashara ndogo, mama lishe kuhusu upatikanaji wa maeneo, imebainika kuwapo mchezo ‘mchafu’ wa wafanyabiashara wakubwa kutumia mgongo wa wamachinga, kusambaza na kuuza bidhaa zao maeneo yasiyoruhusiwa.
Katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, imebainika yako maghala 12 ya bidhaa za chakula eneo la Ubungo, ambako wafanyabiashara ndogo wamekuwa wakigawiwa bidhaa kuziuza maeneo yasiyoruhusiwa na kisha jioni hupeleka hesabu kwa matajiri kwa ujira mdogo.
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera alisema wamebaini tatizo hilo na wanapaswa kulizingatia wakati wa kutekeleza mpango wa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wa kusaidia wamachinga kufanya biashara zao kwa amani kwenye maeneo yanayoruhusiwa.
Aidha, katika kutekeleza azma hiyo ya Tamisemi, Manipsaa ya Ilala imeainisha maeneo kadhaa, ikiwemo Viwanja vya Jangwani ambako itajengwa miundombinu kama vile vyoo, taa na kuwekewa ulinzi, litumike kwa ajili ya soko la kila siku.
Hatua hizo za halmashauri za jijini Dar es Salaam, ni utekelezaji kwa vitendo mpango aliosema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika mkutano wa 18 wa Bunge ulioahirishwa hivi karibuni.
Pinda alisema kimeundwa kikosi cha kiofisi kitakachohusisha wajasiriamali hao kwa lengo la kukubaliana kuhusu maeneo na muda muafaka wa kuendesha shughuli zao.
HABARILEO
MADEREVA wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) wamelalamikia shirika hilo kuwapunguza kazini hivi karibuni bila kufuata utaratibu unaofaa, ikiwa ni pamoja na mchanganuo wa malipo yao.
Wakizungumza na gazeti hili jana, madereva hao walilalamikia shirika hilo kuvunja mkataba waliowekeana na kampuni hiyo ambao ni wa miaka miwili na kuamua kutafuta sababu za kuwasimamisha kazi.
Baadhi ya madereva walikuwepo katika ofisi za UDA zilizoko Kamata, Ilala walisema wameshangazwa na shirika hilo kuwatafutia sababu wafanyakazi za kuwafukuza kazi na kupuuza haki zao.
“Awali tulikuwa tukifanya kazi kwa utaratibu wa dereva wawili kwa gari moja ambapo leo ukiwa kazini kesho yake unapumzika na mwenzako anaingia kazini, lakini ghafla tulibadilishiwa utaratibu mwezi huu ikawa kila gari dereva ni mmoja tu ambaye anatakiwa kufanya kazi siku tano mfululizo,”:-Simon Kamwela.
Alisema hata hivyo walipewa fomu ambazo ni za hiari za kusaini ambayo zimeshajazwa zilizokuwa zinawataka kukubali mfumo huo wa kuendesha gari siku tano mfululizo katika wiki na pia kukiri kupeleka mapato ya kampuni kama dereva alivyopangiwa kila siku.
Madereva hao wanadai kuwa baada ya kufukuzwa kazi barua wamepewa kuanzia Februari 10 mwaka huu na wengine wanaendelea kupewa mpaka sasa wakati barua zinaeleza kuwa wamepunguzwa kazi toka Februari 9 mwaka huu.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook