MTANZANIA
Jeshi la Polisi nchini limetangaza kuanza uchunguzi dhidi ya vikundi vyote vya ulinzi na usalama vinavyoanzishwa na vyama vya siasa nchini.
Pamoja na hili limesema kuwa litachunguza kwa kina mafunzo yanayotolewa na vyama hivyo kama yanahusiana na shughuli za kijeshi au laa.
Hatua hiyo ya Jeshi la Polisi imekuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuzindua kikundi cha Ulinzi na Usalama (Red Brigade) katika mikoa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu alisema kuwa, sheria za nchi zimeweka wazi namna ya kuwapo kwa vikundi vya ulinzi na usalama na si kila mtu anaweza kuanzisha kikundi chake.
IGP Mangu alisema hatua ya kila chama kuanzisha kikundi chake inaweza kusababisha vurugu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
“Kuanzishwa kwa vikundi vidogodogo ndani ya vyama vya siasa ambavyo vinafanya kazi ya ulinzi na usalama vinaweza kuhatarisha amani ya nchi, lazima tuchunguze ili tuweze kubaini mafunzo wanayopewa kama yanafanana na vikosi vya ulinzi na usalama au la, hapo tutajua ukweli zaidi,” IGP Mangu.
MTANZANIA
Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Rwanda, Paul Kagame wamekutana ana kwa ana nchini Kenya.
Hatua hiyo imekuja huku ikiwa imepita miaka miwili tangu Tanzania na Rwanda ziingie katika vita ya maneno hasa baada ya Rais Kikwete kumshauri Kagame kukaa meza moja na kikundi cha waasi cha FDLR cha nchini humo.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa Rwanda wakati akizungumza katika kikao cha Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, ambao ulikuwa ukijadili suala la amani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na ukanda wa Maziwa Makuu.
Ushauri huo pia uliwagusa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), ambao aliwataka kufanya mazungumzo na waasi wanaopingana na serikali zao.
Hata hivyo hali ilionekana kuwa tofauti kwa viongozi hapo juzi katika mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika Jijini Nairobi nchini Kenya, ambapo Rais Kikwete alikabidhi uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika mkutano huo ambao ulikuwa ukiongozwa na Rais Kikwete, muda wote Kagame alikuwa ni mwenye tabasamu dhidi ya kiongozi huyo wa Tanzania.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza mpango maalumu wa wapenzi na wanachama wa chama hicho kuchangia Sh10,000 kwa mwezi ili kupata fedha za kutosha kukiendesha chama ikwa lengo la kuiondoa CCM madarakani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa njia ya kura.
Mbowe alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia mamia ya wakazi na wafuasi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.
Akifafanua kuhusu michango hiyo kwa kutumia mfano alisema, kama eneo la Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini watapatikana watu milioni moja watakuwa wamechanga kwa mwezi Sh100 milioni ambazo zinatosha kuing’oa CCM katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Mbowe alisema, Chadema imefanikiwa kuiteka mikoa yote muhimu katika nchi ambayo ipo vizuri kiuchumi na kukubaliwa na wananchi, hivyo njia ni nyeupe kwa upinzani kuingia Ikulu.
Mbowe alisema kutokana na fursa hiyo Chadema kukubaliwa na taifa hili na CCM kupoteza mwelekeo ndiyo sababu ya wao kushinda uchaguzi.
MWANANCHI
Polisi wenye silaha na mabomu ya machozi pamoja na maofisa usalama, jana walitanda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuzuia vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wasimwone mwenyekiti wao, George Mgoba, aliyelazwa baada ya kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana.
Pamoja na hatua hiyo vijana wengine watatu akiwamo katibu wa wahitimu hao walikamatwa na polisi na walikuwa wanashikiliwa katika Kituo Kikuu jijini Dar es Salaam.
Mgoba Jumatatu iliyopita alitekwa, kuteswa na baadaye kutupwa kichakani katika eneo la Picha ya Ndege, Kibaha mkoani Pwani.
Jana, wahitimu hao wa JKT wanaokadiriwa kufikia 200 walifika katika lango la Hospitali ya Muhimbili saa 11.50 asubuhi na kujichanganya na watu wengine waliokuwa wakisubiri kuwaona wagonjwa wao.
Ilipofika saa 12.10 magari ya polisi matano kila moja likiwa na askari sita yalifika katika eneo hilo na kuingia ndani ya eneo la hospitali hiyo huku polisi waliovaa sare wakisimama kwenye lango hilo kulinda usalama.
MWANANCHI
Jaji Mkuu Mohamed Chande amesema hatma ya majaji wawili waliotajwa kupokea fedha zinazohusishwa na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, itachukua muda mrefu kwa kuwa uchunguzi huhitaji muda mrefu kukamilika.
Jaji Chande ametoa kauli hiyo wakati leo watumishi wa umma na wanasiasa wengine waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo wakifikishwa mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua nembo ya miaka 60 tangu kuanzishwa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Jaji Chande alisema kamati hiyo imeanza kushughulikia tuhuma za kinidhamu na kimaadili dhidi ya majaji hao.
Majaji hao ni Aloysius Mujulizi anayedaiwa kupata Sh40.4 milioni na Prof. Eudes Ruhangisa anayedaiwa kupata Sh400.25 milioni kutoka kwa James Rugemalira wa VIP Engineering.
Jaji Mkuu alisema kamati hiyo ambayo ilianza uchunguzi huo Januari 26, 2015, ikimaliza kazi yake itakabidhi taarifa kwa Tume ya Utumishi ya Mahakama na baadaye kwa Tume ya Uchunguzi wa Kikatiba ambayo yeye ni mwenyekiti.
“Baada ya sisi kupata taarifa na kuipitia ndiyo tutampelekea Rais Jakaya Kikwete kwa maamuzi zaidi na kazi hii siyo ya haraka kwani inahusu haki na maadili,” alisema.
NIPASHE
Visiwa vya Zanzibar vimekumbwa na upungufu wa mafuta ya petrol kwa muda wa siku tatuhali iliyopelekea usumbufu mkubwa kwa wasafiri na wamiliki wa vyombo hivyo vya moto.
Foleni kubwa ilitokea katika baadhi ya vituo vya kuuzia afuta hayo huku wamiliki wa vyombo vya moto wakilalamika juu ya usumbufu wanaoupata kutokana na kukosekana kwa mafuta.
Wasafiri wa daladala pia wamekuwa wakilalamika kupungua kwa usafiri huo na kuchukua muda mrefu kusubiri,
Sababu za kupungua kwa mafuta hayo hazijawekwa wazi na taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa zimetokana na mvutano wa kupungua bei ya mafuta kama ilivyo Tanzania bara tangu kutangazwa kushuka kwa bei hiyo katika soko la dunia.
NIPASHE
Watu wawili wameuawa katika tukio la ujambazi wa kutumia silaha lililohusisha uporaji wa Sh. milioni nane, mali ya akinamama wajasiriamali waliojiunga kwenye Vicoba, jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo lililotokea jana, majambazi wanne wakiwa na silaha wakitumia pikipiki, walimpiga risasi ya mguuni dereva wa bodaboda aliyekuwa katika harakati za kuziokoa fedha hizo na kusababisha kifo chake wakati akikimbizwa hospitalini kutokana na kuvuja damu nyingi.
Tukio hilo la ujambazi lilitokea jana saa 2:30 usiku na kuendelea kwa takriban nusu saa katika eneo la Vijibweni, karibu na mahali linapojengwa daraja la Kigamboni, wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa majambazi hao alikamatwa na wananchi na kushambuliwa hadi kufa, huku wenzake watatu wakifanikiwa kutokomea kusiko julikana.
Hata hivyo, sanduku ambalo lilipatikana baada ya kuuawa kwa jambazi huyo, lilikutwa likiwa na Sh. 700 na nyaraka za kikundi hicho na baadhi ya raia katika eneo hilo waliwatuhumu polisi kwamba ndiyo waliochukua fedha hizo kutokana na mazingira tata ya upotevu wa fedha hizo.
Mmoja wa wanachama wa kikundi hicho cha Vicoba chenye wanachama 30, Amanda Mushi, alisema hadi sasa haijulikani aliyechukua fedha hizo kwani jambazi aliyekuwa na sanduku hilo aliuawa na wananchi baada ya kukimbilia kwenye makazi ya watu na wenzake watatu kutokomea kusikojulikana.
HABARILEO
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ameomba aombewe afanye vizuri asipeleke aibu nyumbani, kwa kile alichoeleza wizara anayoongoza ni ngumu.
Alisema ugumu wake unatokana na wizara hiyo kubeba rasilimali za nchi.
“Niombeeni kwa Mungu, wizara hii inahusika na rasilimali za nchi, ni wizara nzito, kazi ni kubwa tunalinda mafuta, madini, gesi na umeme, sioni sababu ya kujisifu wala kustahili kuliko wengine.
Mnisaidie kwenye maombi ili nifanye vizuri nisilete aibu nyumbani,” alisema. Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe mkoani Dodoma, alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Mpwapwa na wapiga kura wake, waliojitokeza kumlaki na kumpongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Alisema kuteuliwa kushika wadhifa huo ni jambo moja na anahitaji maombi aweze kutekeleza wajibu, kutokana na wizara hiyo kubadilishwa mawaziri na manaibu waziri kila mara.
Alisema kwenye wizara hiyo kuna watu wanaotaka vitalu, kuna watu wanaopora maeneo na wanaotaka kupora mali za Watanzania, licha ya wao pia kuwa watanzania.
“Pamoja na kulinda mali za Watanzania nina wajibu wa kuhakikisha nishati inapatikana kwa watu wote na sasa serikali iko katika mpango kamambe wa kusambaza umeme vijijini,” alisema.
Alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vinakuwa na umeme kwa lengo la kuwafanya Watanzania kuwa na maisha bora. Licha ya kukabidhiwa zawadi mbalimbali wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kibakwe, pia wazee walimkabidhi Sh 100,000 kwa ajili ya kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea tena ubunge jimboni humo.Aidha, viongozi wa dini walimfanyia maombi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook