MWANAHABARI
Serikali ya Kenya imetoa onyo kali kwa makandarasi wa China Communications and Constructions company wasithubutu kushiriki mahusiano ya ngono na wanawake wa nchi hiyo kisha kuwapa ujauzito na kuwaacha wakilea watoto wasio na baba.
Wakinamama wa Mombasa wamekuwa wakitajwa kuwa karibu na makandarasi hao wakati wa mradi wa ujenzi wenye urefu wa kilomita 2,935 kutoka bandarini Mombasa hadi mjini Kigali kupitia Nairobi kisha Malaba, Kampala Uganda.
Msemaji wa Shirika la Reli la Kenya Mary Oyuke alisema wachina hao wamewekewa mipaka ya mahusiano na wenyeji hususan wa maeneo ambapo mradi huo unapita.
Wachina watagharamia mradi huo kwa asilimia 90 wakati wa awamu ya kwanza ya mradi kutoka Pwani hadi Nairobi umbali wa km 610 ambao ulianza tangu oktoba mwaka jana.
MWANANCHI
Kanisa Katoliki nchini limeanza rasmi mkakati wa kutoa elimu kuhusu Katiba Inayopendekezwa kwa waumini wake, kutokana na kuondolewa kwa mambo mengi ya msingi yaliyotolewa maoni na wananchi.
Mkakati huo umeanzia katika Jimbo la Mwanza ambapo imedaiwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Juda Thaddeus Ruwai’chi ameunda kamati maalumu iliyopewa jukumu la kuchambua na kutoa ufafanuzi juu ya Katiba Inayopendekezwa katika makanisa yaliyopo katika jimbo hilo kupitia semina mbalimbali.
Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba hiyo inatarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu (siku 45 kuanzia leo), katika mkakati huo kanisa hilo limeainisha mambo 100 yaliyotolewa maoni na wananchi lakini yakaondolewa.
Uongozi wa kanisa hilo umekiri kuwapo kwa maelekezo hayo yakiwa na lengo la kutoa elimu kwa waumini wake kuhusu mambo yaliyomo na yasiyokuwamo kwenye Katiba Inayopendekezwa.
Kanisa hilo kupitia Tume ya Haki na Amani ya Tec limekuwa linatoa matamko mbalimbali kuhusu mchakato huo, likiwamo lile la Machi mwaka jana la kupendekeza Serikali tatu, lililosababisha Askofu Mkuu wa Jimbo Mkuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuibuka siku mbili baadaye na kusema msimamo huo siyo wa Kanisa Katoliki nchini.
Akifafanua tamko hilo siku mbili baadaye, Kardinali Pengo, alisema “Maoni ya Tume hayawezi kuwa ni msimamo wa kanisa. Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kutoa misimamo yake na huwa inatolewa na Mwenyekiti wa TEC.”
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu mpango huo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, alisema lengo la mkakati huo ni kuhakikisha waumini wa kanisa hilo wanaijua katika hiyo ili waweze kupiga kura.
NIPASHE
Kuna kila dalili kwamba uhamisho wa Waziri Dk. Harrison Mwakyembe kutoka Wizara ya Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki, akibadilishana nafasi na Samuel Sitta, ni sehemu ya kumwepusha na kadhia ya kashfa ya mabehewa feki ambayo hadi sasa imegundulika kuwa ni kashfa nyingine inayoitafuna Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
Uchunguzi huru umegundua kuwa hatua ambazo zilianza kuchukuliwa na Sitta katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA), nako TRL zimeanza kutikisa baada ya kubainika kwamba mabehewa ambayo yaliingizwa nchini kutoka China na kupokelewa na Dk. Mwakyembe kwa mbwembwe zote kisha kubainika hayana viwango, wakubwa wa kampuni hiyo walijua hilo, lakini wakafunika kombe kwa kuwa wakubwa walipeana zabuni kwa njia ya kujuana.
Habari zinasema kamati iliyoundwa na Sitta kuchunguza kashfa ya uingizaji mabehewa hayo kutoka India, tayari imeibua mambo mazito ambayo yanaongeza orodha ya kashfa za ulaji na ufujaji wa fedha za umma uliosimamiwa na baadhi ya viongozi wa serikali wakitumia madaraka yao vibaya.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka TRL, uingizaji wa mabehewa hayo ulifanywa na Kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited ya India kwa kushirikiana na mfanyabiashara mmoja nchini ambaye kwa miaka mingi amehusika katika kadhia nyingi za kujipatia fedha kwa mikataba laghai dhidi ya serikali na mashirika yake.
Vyanzo vyetu ndani ya TRL vinasema kuwa kamati iliyoundwa kuchunguza kashfa hiyo ya ufisadi wa mabilioni ya fedha, inatarajia kukamilisha taarifa yake ya uchunguzi hivi karibuni na kuikabidhi kwa Waziri Sitta, lakini tayari imegundua madudu mengi ikiwamo wakubwa kupokea mabehewa yenye hitilafu wakati wakijua.
Waziri Sitta amesema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia jambo lolote hadi atakapokabidhiwa ripoti ya uchunguzi.
“Suala la mabehewa feki nimelikuta na kuna tume (kamati) iliundwa kuchunguza na inatarajia kukamilisha ripoti yake hivi karibini, nadhani kwa sasa tungevuta subira ila niwahakikishie wananchi sitaogopa kuchukua hatua bila kujali kashfa hiyo inamhusu mtu au kiongozi wa namna gani,” -: Sitta.
Kashfa ya uingizaji wa mabewa feki iligundulika mwishoni mwa mwaka jana, ikidaiwa kuwa kuna ufisadi mkubwa umefanyika ndani ya TRL katika utoaji wa zabuni ya ununuzi wa mabehewa mapya.
NIPASHE
Mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa,Khalid Kangezi, anahojiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, kwa tuhuma za kushiriki katika mipango ya kukihujumu chama hicho na kutaka kumdhuru Dk. Slaa.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Camillius Wambura, alithibitisha jana Kangezi kufikishwa katika kituo cha polisi Oysterbay na kwamba, hadi jana jioni alikuwa akiendelea kuhojiwa.
Taarifa za awali zilizotolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, zilieleza kuwa Kangezi amekuwa akitumiwa na maofisa 22 wa vyombo vya usalama katika miaka miwili iliyopita kufanya mipango hiyo dhidi ya chama hicho.
Marando alidai mipango hiyo imegunduliwa na kitengo cha usalama cha Chadema kupitia simu za Kangezi na kwamba, ililenga kuiumiza Chadema kisiasa.
Alidai katika hujuma hizo, Kangezi amekuwa akiwasiliana na mmoja wa vigogo wa ngazi ya taifa wa CCM.
Marando alidai kuanzia Desemba, mwaka jana hadi wiki iliyopita, Kangezi alikuwa amekwishafadhiliwa Sh. milioni saba kwa ajili ya matumizi ya mawasiliano ya simu kufanikisha upatikanaji wa taarifa za Chadema kupitia vikao vyake mbalimbali, ikiwamo kamati kuu.
“Huyu kijana ilibidi atuandikie statement (andishi) kwa mkono wake mwenyewe. Na pamoja na mambo mengine juu ya mheshimiwa (kigogo wa CCM-anamtaja jina). ‘Mzee (anamtaja jina) mwenye simu namba (anaitaja) mimi nilimpigia mara tatu, amenitumia fedha za vocha mara mbili kiasi cha Sh. 50,000 siku ya Jumatatu tarehe 14/7/2014 na pia 150,000 tarehe 4 Desemba, 2014 siku ya Alhamisi kwa madhumuni ya kunishawishi kumpatia taarifa za siri za chama na pia kumpigia simu katika vikao mbalimbali,” alidai Marando.
MTANZANIA
Zaidi ya raia 500 wameizingira nyumba moja iliyokuwa imewafungia ndani watoto 18 wenye umri kati ya miaka mitatu na 17 mjini Moshi.
Watoto hao inadaiwa walifungiwa kwenye nyumba hiyo yenye vyumba vinne na choo kimoja ambapo inadaiwa walikuwa wakifundishwa masomo ya dini.
Taarifa za kuwapo kwa watoto hao zilibainika juzi jioni mjini hapa hali iliyovuta hisia za wakazi hao, huku wengi wao wakitaka kujua lengo la watoto hao kuwa eneo hilo na hali zao kiafya.
Hali hiyo ililazimu Jeshi la Polisi kuingilia kati na kuimarisha ulinzi ambapo waliwatoa watoto hao, huku wakitawanya wananchi hao waliokuwa wameizingira nyumba hiyo.
Chanzo cha kuaminika kilidia kuwa watoto hao waliokusanywa katika nyumba hiyo wanatoka katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Mwanza.
Akizungumza na wananchi waliokuwapo eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga, alisema walipata taarifa ya kuwapo kwa watoto hao kutoka kwa msamaria mwema.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema kitendo cha kuwakusanya watoto sehemu moja bila kibali ni kinyume cha sheria.
“Mafunzo anayoyatoa kwa watoto hawa, hata kama ni ya dini, ni lazima yafuate taratibu za nchi. Sheria zipo, unapokusanya watoto mahala pamoja kunatakiwa kuwaje kuanzia mazingira hadi eneo lenyewe na kama una taasisi unaendesha mafunzo, je kituo kimesajiliwa? Na ndiyo maana tumeagiza watoto warudishwe kwa wazazi wao,” Makunga.
Kwa upande wake, mmiliki wa nyumba hiyo, Abdulnasir Abdulrahman, alisema wamewakusanya watoto hao ili kuwafundisha masomo ya dini ya Kiislamu na kuwakuza katika imani hiyo wakiwa wadogo.
“Watoto wote tunaoishi nao hapa wana wazazi wao, ambao wamekubaliana na sisi waendelee kupata elimu hiyo hapa chini ya uangalizi wetu na wazazi wao wamekubaliana kuwalea,” Abdulrahman.
MTANZANIA
Matumizi ya kila siku ya dawa za kupunguza maumivu za paracetamol huongeza hatari ya ugonjwa wa moyo, kiharusi na kufupisha maisha ya binadamu, utafiti mpya umeonya.
Paracetamol hupendelewa zaidi na madaktari wengi hudai zi salama kulinganisha na aspirin, ambayo imehusishwa na kuvuja damu tumboni na ibuprofen iliyohusishwa na magonjwa ya moyo na kiharusi.
Lakini watafiti wa Uingereza waliofanya uchunguzi huo uliowahusisha wagonjwa 666,000 wanasema hatari iliyomo katika dawa hizo huenda ilipuuzwa na sasa wameagiza uchunguzi ufanywe kuhusu usalama wake.
Taarifa hizo iwapo ni za uhakika, itakuwa pigo kwa wengi kwa vile paracetamol zimezoeleka kuliko dawa nyingine yoyote ile ya kupunguza maumivu, na inapatikana kirahisi na kila mahali.
Zaidi ya hayo, makasha milioni 200 ya paracetamol huuzwa kila mwaka.
Hata hivyo, Prof. Philip Conaghan wa Taasisi ya Dawa ya Rheumatic and Musculoskeletal mjini Leeds, Uingereza, amefichua kuwa matumizi ya muda mrefu ya paracetamol yana athari mbaya kiafya.
Professa Conaghan alipitia tafiti nane zilizofanyika huko nyuma kutathimini uhusiano baina ya matumizi ya muda mrefu ya paracetamol na matatizo ya kiafya kwa watu wazima.
Utafiti huo umebaini wagonjwa wanaopewa dawa hizo za kupunguza maumivu mwilini kwa muda mrefu wana hatari kubwa ya asilimia 63 kufupisha maisha yao.
Hatari ya kupatikana ugonjwa wa moyo na kiharusi iko juu kwa asilimia 68, huku pia kukiwa na hatari kubwa ya asilimia 50 ya kupatikana vidonda vya tumbo au hata kuvuja damu.
Watafiti hao walihitimisha kuwa kutokana na ukubwa wa matumizi ya paracetamol na urahisi wa upatikanaji, uchunguzaji wa athari zinazoweza kupatikana kutokana na dawa hizo ulipuuzwa.
MTANZANIA
Mchungaji kiongozi wa kanisa la ufufo na uzima Josephat Gwajima, amesema viongozi wa dini hawawezi kujitenga na siasa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu katika jamii.
Gwajima alitoa kauli hiyo wakati akitunukiwa tuzo ya heshima ya udaktari kutoka katika chuo kikuu cha Biblia na Theolojia cha Omega Global ‘OGU’ cha Afrika Kusini,jijini Dcar es salaam juzi.
Alisema kumekuwa na dhana kwamba viongozi wa dini kujihusisha na siasa ni kwenda kinyume na kazi wanayoifanya.
“Huwezi kutenganisha siasa na dini,kwa sababu siasa inahusu watu na dini inahusu watu,kwa hiyo ni vitu vinavyotegemeana,watu wanaosema kwamba viongozi wa dini wakijihusisha na siasa ni kupotoka si kweli”- Gwajima.
MTANZANIA
Umoja wa Vijana wa Chama cha NCCR-Mageuzi, umempitisha Dk. George Kahangwa ambaye ni muhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es salaam kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho ambaye atachuana na wagombea wengine watakaopitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Uamuzi wa kumpitisha mgombea huyo umekuja baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, kudai kuwa hatogombea tena nafasi hiyo kwa sababu anakwenda kugombea ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa vijana wa NCCR-Mageuzi, Deo Meck, alisema kikao kilichofanyika Machi 5, mwaka huu, kilifikia uamuzi huo baada ya kuona Dk. Kahangwa ana vigezo vya kuwania nafasi hiyo.
“Tulikaa kwenye vikao halali vya chama na kuamua kwa pamoja kupitisha jina la Dk. George Kahangwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, jambo ambalo limetufanya tuutangazie umma.
“Kutokana na hali hiyo, tutamuunga mkono mgombea wetu hata kwenye mchakato wa kupitisha jina la mgombea wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa sababu tunaamini ana vigezo vya kuongoza taifa hili,” Meck.
Aliongeza kutokana na hali hiyo, wamewaomba wajumbe wengine kutoka Ukawa kuungana nao ili kuhakikisha mgombea huyo anachaguliwa kuwa mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
HABARILEO
Licha ya Serikali,jamii na jumuiya ya kimataifa kukemea ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), bado kuna wanaoendelea kung’ang’ania mila potofu za kuamini kwamba bila ya ushirikina unaohusishwa na matumizi ya viungo vya albino, hawawezi kufanikiwa kimaisha, iwe katika kisiasa au kibiashara.
Hayo yanathibitishwa na kuendelea kuripotiwa kwa matukio ya ukatili dhidi ya albino, ambapo usiku wa kuamkia jana, watu wasiojulikana walimshambulia na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita, Baraka Cosmas na kisha kutokomea nacho kusikojulikana.
Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas Yoram (32) na Prisca Shaaban.
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda alisema tukio hilo ni la saa 8 usiku wa kuamkia Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake huku Baba wa mtoto huyo hakuwepo wakati huo.
Akielezea zaidi, Kamanda Mwaruanda alisema usiku huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada ya kukataa kuwapatia mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.
“Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi vibaya … “Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojuliakana,” alibainisha.
Aliongeza kuwa wakati hayo yakitokea, baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, mtoto huyo amelazwa katika katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama yake mzazi.
“Watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo hicho cha kiganja cha mkono wa mtoto Baraka,” alisisitiza Kamanda.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook