MWANANCHI
Machungu ya Watanzania yakiwa hayajapoa kutokana na kashfa ya Sh306 bilioni kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ufisadi mwingine wa zaidi ya Sh252 bilioni umeibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad ndani ya wizara ya ujenzi.
Ukaguzi maalumu uliofanywa na ofisi ya CAG katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12 umebaini kuwa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, bungeni Novemba 2013 kuwa fedha hizo zilitumika kwa miradi ya ujenzi wa barabara, haikuwa sahihi.
Kutokana na ufisadi huo, habari zilizolifikia Mwananchi zinasema CAG amependekeza hatua stahiki zichukuliwe kwa wahusika wa wizara ya ujenzi na wakala wa barabara ili kuleta imani na uwazi katika bajeti kwa jamii na wahisani.
“Wizara ya ujenzi ililidanganya Bunge kuwa kuna ujenzi wa barabara hizo wakati wakijua kwamba walikusudia kulipa madeni ya wakandarasi na washauri wa ujenzi wa barabara…mpango mkakati wa wakala wa barabara wa mwaka wa fedha 2011/12 pamoja na manunuzi ulioidhinishwa havikuonyesha utekelezaji wa mradi huo,” chanzo cha habari kilikariri ripoti ya CAG.
Matumizi hayo yasiyo sahihi yaliibuliwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Novemba 22, 2013 baada ya kutilia shaka kiasi hicho cha fedha na ofisi ya CAG kuagizwa kufanya ukaguzi.
Katika kikao hicho ambacho wizara ya ujenzi iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake wa wakati huo, Balozi Herbert Mrango alihojiwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa CAG mwaka 2011/12.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya mwaka huo Sh348.1 bilioni zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililokuwa limetajwa kuwa ni la mradi maalumu hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa bungeni.
“Ni vizuri leo (ilikuwa Novemba 22 mwaka 2013) uiambie kamati fedha hizi ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa jambo gani. Tunajua kwamba fedha hizi zilipunguzwa Sh95 bilioni na kupelekwa Wizara ya Uchukuzi, zilibakia Sh252.975 bilioni katika kifungu hicho lakini kuna bilioni 100 zimetumika visivyo,” Zitto.
Alisema katika majumuisho ya bajeti wizara hiyo, Dk Magufuli na Dk Harrison Makyembe aliyekuwa Naibu waziri wa wakati huo aliyekuwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi walitoa maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha hizo.
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema analindwa na Mungu na ndiyo maana chama hicho kimegundua mpango wa mlinzi wake kushawishiwa na maofisa usalama wa taifa ili kumwekea sumu katika chakula au maji.
Mlinzi huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay juzi, pia anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM kuiba siri za chama hicho.
Tayari polisi imeanza kuchunguza taarifa hizo na jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura aliliambia gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ana haki kama watuhumiwa wengine wanaofikishwa polisi wakikabiliwa na kesi za jinai na kusisitiza kuwa; “Tuhuma zinazomkabili ni za kawaida na tunazichunguza.”
Akieleza alivyopokea taarifa hizo Dk Slaa alisema, “Ninalindwa na Mungu ndivyo ninavyoweza kusema. Chadema sisi huwa tunaanza na Mungu na kumaliza na Mungu. Ushahidi umewekwa wazi na hili ni jambo la kweli na limenigusa kwa kiasi kikubwa.”
Alisema baadhi ya mambo yaliyofanywa na mlinzi wake ameyaona kwa macho na kusisitiza kuwa njama zinazofanywa na wanaomtumia haziwezi kukiondoa chama hicho katika harakati zake za kila siku.
“Tupo makini ndiyo maana tumebaini yote. Tunawajua waliohusika na tupo makini katika kuwafuatilia. Kama Mungu yupo upande wetu tumuogope nani zaidi,” alisema.
Alisema Chadema ina safari ndefu hivyo ni lazima wana-Chadema kuvaa viatu ili kujikinga na vumbi na uchafu wa kila aina, akimaanisha kuwa chama hicho kinakumbana na vikwazo vingi.
Hili ni tukio la tatu kwa Chadema kudai kuna mipango ya kumfuatilia Dk Slaa, mara ya kwanza ilikuwa Februari 2009 alipobaini kutegewa vinasa sauti hotelini mkoani Dodoma na mkakati uliotajwa kuwa wa kuwaua yeye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
MWANANCHI
Daktari bingwa wa zamani wa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk Fulgence Mosha anasotea mafao yake ya kiinua mgongo na pensheni kwa miaka 10 mfululizo bila mafanikio.
Akizungumza juzi, Dk Mosha alisema licha ya kulifikisha suala hilo kwenye vyombo husika, ikiwamo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, bado mafao yake ni kitendawili.
Dk Mosha aliajiriwa na Serikali mwaka 1983 kabla ya Januari 1,1995 kupelekwa KCMC kwa barua ya Desemba 29, 1994 yenye kumb HE/MP ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Desemba 11, 2004, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikauandikia barua uongozi wa KCMC kutoa kibali cha Dk Mosha kustaafu rasmi baada ya kufikisha umri wa miaka 60 wa kustaafu kisheria.
Alisema baada ya kustaafu, alilipwa Sh10 milioni na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF), ikiwa ni michango yake na ya mwajiri ambaye ni Shirika la Msamaria Mwema (GSF) linalomiliki KCMC.
“Katika utumishi wangu nimefanya operesheni kubwa zaidi ya 7,000 zikiwamo za viongozi wakuu wa nchi hii lakini leo baada ya kustaafu napigwa danadana sina thamani tena kwa Serikali,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Mosha, utata wa mafao yake ikiwamo kulipwa pensheni kila mwezi, unatokana na Hazina kutopeleka mchango wowote katika Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
Dk Mosha alisema baada ya kustaafu, alichukua malipo yake ya NSSF na kuyapeleka PSPF ili yajumlishwe na michango ya Serikali katika kipindi alichokuwa mtumishi wa Umma (1983-1994).
“Zile fedha zilikaa kule, PSPF wakaamua kunirudishia maana Serikali haikupeleka ile michango yake ambayo walitakiwa wailipe kati ya 1983 na 1994 nilipokuwa serikalini,” alisema.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu malalamiko ya Dk Mosha alionyesha kushtushwa na kusema, huenda daktari huyo hakutumia njia sahihi kudai haki yake.
“Simfahamu huyo daktari lakini ni jambo linaloshtua. Naomba mwelekeze aje ofisini na nyaraka zake zote nimpeleke SSRA (Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii),” Kabaka.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi wilayani hapa, limedai kuwa watoto waliokutwa ndani ya nyumba katika eneo la Pasua, Manispaa ya Moshi siyo wakazi wa Kilimanjaro na walikuwa wakiishi kwenye mateso makubwa.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela imeeleza kuwa hayo yalibainika katika mahojiano baina ya watoto na askari wa dawati la jinsia.
Alisema watoto hao wanatoka mikoa mbalimbali ikiwamo Tanga, Mara, Kagera, Mbeya na Dodoma.
Kamanda Kamwela alisema pia wamegundua kuwa watoto walikuwa wakiishi kwenye mazingira magumu ikiwamo kulala chini katika chumba kidogo.
Alisema polisi linawashikilia watu wawili (mume na mke) ambao wanatuhumiwa kuwahifadhi watoto hao.
Kamanda huyo alisema watoto hao wana umri wa kwenda shule, lakini walikuwa hawasomi.
Alisema polisi wanachunguza aina ya masomo ya dini waliyokuwa wakifundishwa.
“Lazima tuchunguze uhalali wa masomo ya dini waliyokuwa wakisoma ili tujue kama kweli watoto hawa walipelekwa na wazazi wao au la, kwa kuwa watoto hao walipaswa kuwa shuleni” Kamwela.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga alisema watoto hao walikuwa wakiishi kwenye mazingira magumu, huku wakipewa adhabu kali ikiwamo kubeba matofali mgongoni pindi wanapokosea.
Alisema kwa wazazi watakaowatambua watoto wao, wanapaswa kwenda na uthibitisho ikiwamo cheti cha kuzaliwa au uthibitisho mwingine utakaoonyesha ni mzazi halisi.
NIPASHE
Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dk. James Benedict Diu, amekiri kupokea mgawo wa zaidi ya Sh. milioni 80.8 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira, huku akitoa maelezo yanayokinzana kuhusu sababu za kupewa fedha hizo pamoja na matumizi yake.
Fedha hizo, ambazo anadaiwa kuingiziwa na Rugemalira katika akaunti yake iliyofunguliwa katika Benki ya Biashara ya Mkombozi tawi la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, zinadaiwa kuwa ni sehemu ya zaidi ya Sh. bilioni 200 zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Dk. Diu, ambaye amewahi kuwa Meneja Udhibiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) mwaka 2006-2011, alitoa maelezo hayo kwa nyakati tofauti wakati akijibu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma zinazomkabili mbele ya Baraza la Maadili jana na kudai kuwa hazijui kazi za Ewura.
Awali, akimhoji shahidi wa upande wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambao ni walalamikaji katika shauri hilo, Zahara Guga, Dk. Diu alidai fedha alizopokea kutoka kwa Rugemalira, hazikuwa zawadi, bali zilikuwa ni msaada zilizotolewa kuchangia gharama za matibabu ya mkewe, Beatrice, ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Sijapokea zawadi, bali ni mchango kama msaada wa matibabu ya mke wangu. Nasisitiza tena hii haikuwa zawadi. Natambua kwamba iwapo ningepokea zawadi ningetamka kwa afisa mas-uul (bosi wake) kwa kuwa ile haikuwa zawadi sikuona umuhimu wa kuitamka,” Dk. Diu.
Wakati awali akieleza fedha hizo ziliwa ni msaada kwa ajili ya kumuuguza mkewe. baadaye wakati akitoa maelezo ya kujitetea mbele ya baraza hilo jana, Dk. Diu alidai fedha alizopewa na Rugemalira zilikuwa ni mkopo wenye masharti nafuu, ambao walikubaliana kwa mdomo aulipe siku yoyote atakapofanikiwa.
Alidai Rugemalira ni rafiki wa karibu na wa siku nyingi yeye na familia yake na kwamba, alihitimu naye Shahada ya Kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1982-1985.
NIPASHE
Baadhi ya wanazuoni, viongozi wa dini, wanasiasa na wanaharakati wamesema hakuna muujiza wowote unaoweza kufanyika hivi sasa kufanikisha kura ya maoni Aprili 30, mwaka huu.
Wamesema kulazimisha kura ya maoni kama ilivyotangazwa ni sawa na ‘kuchochea fujo’, jambo linaloweza kuepukika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, walisema nchi imegawanyika vipande vipande, huku wengine wakipinga mchakato wote, hivyo kulazimisha kura ni kuendelea kuligawa taifa.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Semboja Hajji, alisema kulazimisha kura ya maoni ni sawa na kuleta fujo.
“Hii iko very clear (wazi kabisa), kwamba muda unapingana na jambo hili. Rasilimali muda ni jambo adimu na mimi sizungumzi siasa, ni hali halisi kwamba, muda hauko na sisi kwa sasa. Kwa ushauri wangu, tusilete fujo kulazimisha jambo hili. Unaweza kulazimisha kufanya jambo zuri, lakini mwisho likaonekana halina maana kabisa,” alisema.
Alisema hata kama kura ya maoni haitafanyika sasa hivi, Watanzania wapo na Katiba ni yao, hivyo hakuna mtu au chama chochote kinachoweza kufanikisha jambo hilo kwa sasa.
Dk. Semboja alisema hakuna sababu ya kufanya haraka kwenye jambo kubwa na zito kwa mustakabali wa nchi kwa miaka mingi ijayo na kusema Watanzania watamkumbuka Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa busara wa kuanzisha mchakato huo na hivyo ni busara sasa ikaachwa ili ipate muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kura ya maoni.
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole, alisema serikali haijajiandaa kufanikisha kura ya maoni kwa kuwa nchi imegawanyika na wananchi hawana uelewa wowote kuhusu Katiba inayopendekezwa.
Alisema kabla ya kura ya maoni, taifa linahitaji muda zaidi kujenga muafaka na kuelimishana kuhusu maudhui yaliyomo kwenye Katiba inayopendekezwa na namna ilivyopatikana.
Alisema siyo busara kwa nchi kuendelea na mchakato huo na hata kufika kwenye kura ya maoni ikiwa vipande vipande kama ilivyo sasa na kwamba, muda huo kwa sasa haupo.
“Tangu Katiba inayopendekezwa itolewe, Watanzania hawajaelimishwa vya kutosha juu ya maudhui, wala iliyopelekea kupatikana kwa rasimu hiyo kwamba, ni zao la kitu gani…Katiba hii inapaswa ipimwe na iliyokuwa rasimu ya tume ya Warioba siyo kwa katiba ya mwaka 1977 kama baadhi ya watu wanavyoeleza. Hatuwezi kwenda kwenye kura Aprili 30,” alisema.
Alisema hata elimu kwa umma iliyopaswa kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni, bado haijatolewa na kwamba, hata asasi za kiraia, ambazo zilitakiwa kushiriki kutoa elimu hiyo, nazo bado hazijaanza kazi.
MTANZANIA
Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakidaiwa kutoa mafunzo ya ugaidi kwa vijana wa Tanzania mkoani Tanga.
Mmoja wao anaelezwa kuwa alikuwa pia akitoa mafunzo ya jeshi kwa kundi la Hizbul al lililotaka kuipindua serikali ya Somalia mwaka 2010.
Washtakiwa hao, Ally Nassoro na Juma Zuberi walifikishwa jana katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Njike akisoma mashtaka ya washtakiwa, alidai kati ya Oktoba Mosi, 2010 na Januari 30, 2001, katika eneo la Doblen Kisimayu, Somalia, Nassoro aliwezesha watu kushiriki mazoezi ya jeshi ya kundi la Hizbul al, lengo likiwa ni kuipindua Serikali ya Somalia.
Nassoro pia anadaiwa kati ya Mei Mosi, 2013 na Agosti 31, mwaka jana, katika Msitu wa Nguu ulioko eneo la Gombe wilayani Muheza, Tanga, aliwapa mafunzo ya matumizi ya silaha watu ambao hawakuwapo mahakamani hapo, lengo likiwa ni kufanya ugaidi nchini.
“Shtaka la tatu linamkabili Zuberi. Anadaiwa kati ya Mei Mosi, 2013 na Agosti 23, mwaka jana katika Msikiti wa Kichangani, Magomeni, Dar es Salaam, alimsaidia Ally Nassoro kutekeleza vitendo vya ugaidi kwa kumpa sehemu ya kukaa na kutekeleza mipango yake.
“Zuberi unadaiwa katika kipindi hicho ukiwa na eneo la biashara katika Msikiti wa Kichangani, Magomeni, ulimruhusu Ally Nassoro kukaa na wenzake kupanga na kujadili mipango ya mafunzo kwenye Msitu wa Nguu kutekeleza vitendo vya ugaidi,” Njike.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine.
MTANZANIA
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa miezi mitatu kwa Msajili wa Hazina kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa shirika jipya la ndege litakaloendeshwa na mamlaka za hifadhi za taifa ili kutoa huduma kwa abiria na watalii
Mamlaka hizo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Akizungumza na wadau katika kikao cha majadiliano kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema mamlaka hizo zitashirikiana moja kwa moja na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili kuangalia namna ambayo shirika hilo linaweza kufanya kazi zake, hivyo kusaidia Serikali kuongeza mapato.
“Lengo letu ni kuhakikisha Serikali inamiliki ndege zake binafsi ambazo zitaweza kubeba abiria na watalii wanaokuja nchini, hivyo kusaidia kuongeza mapato,” Zitto.
Mwenyekiti huyo wa PAC alisema mchakato wa uanzishwaji wa shirika hilo ulianza mwaka 2011 ambapo wabunge kwa pamoja waliangalia namna ya kulishughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuzitaka mamlaka hizo kuanzisha mashirika ya ndege ili yaweze kufanya kazi hiyo.
Alisema ilipofika Novemba 2012, wabunge hao walifikia maazimio ya kuitaka Serikali kutekeleza maagizo yaliyotolewa na wabunge ili kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa.
Zitto alisema kutokana na hali hiyo, Serikali iliziandikia barua mamlaka hizo na kuwataka kuchangia uanzishwaji wa shirika hilo jipya bila ya kumiliki jambo ambalo ni kinyume na maazimio ya wabunge.
“Kwa mwaka wanatoa wastani wa Sh bilioni 15 za pato ghafi kwenda hazina, halafu wanatoa asilimia 3 ya mapato yao kwa ajili ya kupeleka Wizara ya Maliasili na Utalii na asilimia 30 kwa ajili ya kodi,” alisema Zitto.
Alibainisha wakati wanaangalia namna ya kulishughulikia suala hilo kamati hiyo ilikaa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuangalia namna ambayo wanaweza kulishughulikia suala hili.
HABARILEO
Wakazi 10 wa jijini hapa, akiwemo mwanafunzi wa sekondari wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wakikabiliwa na makosa matano tofauti kuhusu tukio la kuwanyang’anya polisi silaha pamoja na kumuua askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Sajenti Mohamed Rashid Kajembe.
Mwanafunzi aliyefikishwa mahakamani ni Rajab Bakari (19) wa shule ya sekondari na mkazi wa Makorora jijini hapa.
Watuhumiwa tisa wameelezwa kuwa ni wafanyabiashara, nao ni Mbega Seif (25) maarufu ‘Abuu Rajab’ mkazi wa Kiomoni, Amboni, Ayubu Ramadhani (27) maarufu ‘Chiti’ ambaye ni fundi umeme na mkazi wa Kona Z Kiomoni, Hassani Mbogo (20) maarufu ‘Mpalestina’ mkazi wa Makorora, Mohamed Ramadhani (19) mfanyabiashara na mkazi wa Makorora, Sadiki Mdoe (25) maarufu ‘Kizota au Kisaka’ mkazi Magaoni. Washtakiwa wengine ni Saidi Omari (26) mkazi wa Magaoni Tairi Tatu, Nurdin Mbogo (27) Makorora, Ramadhan Mohamed (18) mkazi wa Donge pamoja na Omari Harubu Abdala (55) maarufu ‘Ami’ mkazi wa Dunia Hoteli Makorora.
Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Aziza Rutala, Wakili wa Serikali, George Barasa akisaidiana na MariaClara Mtengule, walidai kuwa kosa la kwanza hadi la tatu linawahusisha washitakiwa namba moja mpaka nane (1 8) ambao wanatuhumiwa kushiriki kula njama ya kutenda kosa kinyume cha sheria.
Barasa alidai kuwa katika maeneo tofauti ya jijini Tanga kati ya Septemba mosi 2014 hadi Januari 26 mwaka huu, washitakiwa wote wanane kwa pamoja walitenda kosa la kula njama na kufanya kosa la unyang’anyi wa silaha.
Katika kosa la pili, Barasa alidai mahakamani hapo kwamba mnamo Januari 26 mwaka huu, katika mgahawa wa Jamali ulipo kati ya barabara ya Nne na ya Tano jijini Tanga, washitakiwa wote wanane waliiba silaha moja aina ya SMG namba za usajili 14303545 mali ya Polisi na muda mfupi kabla ya kutenda kosa hilo walitumia visu kumchoma askari H 501 Mwalimu ili kupata silaha hiyo.
Kosa la tatu la washitakiwa hao ni unyang’anyi wa kutumia silaha, na washitakiwa wote wanane wanadaiwa kuwa katika mgahawa wa Jamali uliopo kati ya barabara ya nne na ya tano waliiba silaha nyingine yenye namba za usajili 14301230 SMG mali ya polisi na kwamba muda mfupi kabla ya kutenda kosa hilo walimtishia.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amesema alipoingia madarakani, serikali ilikuwa ikikusanya mapato ya Sh bilioni 170 kwa mwezi, lakini sasa inakusanya Sh bilioni 900 kwa mwezi.
Rais alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua Mkutano wa 22 wa Wahasibu Wakuu wa Ukanda wa Afrika Mashariki na kusini mwa Bara la Afrika (ESAAG), ulioshirikisha nchi 14.
“Nilipoingia madarakani, serikali ilikuwa ikikusanya mapato ya Sh bilioni 170 kwa mwezi, lakini sasa serikali inakusanya Sh bilioni 900 kwa mwezi, lakini kutokana na utawala bora na uwajibikaji, sasa serikali inakusanya Sh bilioni 900 kwa mwezi na hiyo inachangiwa pia na sheria nzuri za usimamizi wa fedha na manunuzi,” alisema Rais ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2005.
Rais aliwataka wahasibu na wakaguzi wa fedha, kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha na kukagua miradi ili iendane na thamani halisi ya fedha zilizotolewa kwa manufaa ya umma.
Pia, aliwataka wahasibu na wakaguzi hao kuzingatia elimu waliyonayo kwa kutoa hati safi, kulingana na ubora, badala ya kutoa hati hizo kwa kujuana au bila kujiridhisha.
Akitoa mfano, alisema kijijini kwake iliwahi kutolewa hatisafi na ilielezwa kuna miradi miwili imetekelezwa, lakini kiuhalisia hapakuwa na miradi hiyo, hali inayoonesha kwamba ukaguzi haukufanyika kwa usahihi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook