MWANANCHI
Mke wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere amesema kuwa mtoto wake, Makongoro Nyerere ana haki ya kugombea nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Ijumaa wiki iliyopita, Makongoro alilieleza gazeti hili kuwa uamuzi wake kuhusu kuwania kiti hicho utajulikana mara kipenga kitakapopulizwa na CCM.
Kauli ya Makongoro ilitokana na uvumi uliokuwa umeenea katika mitandao ya kijamii kuwa mtoto huyo wa tano wa mwalimu Nyerere alikuwa anaandaliwa na watu waliofanya kazi karibu na mwalimu awanie nafasi hiyo.
Mama Maria aliyekuwa ameawaalika waandishi wa habari kuzungumzia uvumi uliosambaa kuwa amefariki dunia, alitoa kauli hilo baada ya kuulizwa kama uvumi huo unahusiana na habari kuwa mwanaye anataka kugombea urais.
Alisema, “Hapana. Hayo mambo hayahusiani na mwanangu kutaka kuwania urais… yeye ni raia wa Tanzania na hiyo ni haki yake ya msingi,”
Pia, alidokeza kuwa wakati akizungumza na mwanaye mwingine juzi baada ya uvumi wa kifo chake, naye alimwambia kuwa anataka kuwania nafasi hiyo.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na uvumi huo alisema kuwa, taarifa za uvumi wa kifo chake zilikuwa za furaha kwake na wala siyo za huzuni kama watu wengi walivyodhania.
“Tumekuwa tukifanya maombi ya kusali na kufunga kwa siku 40 kabla ya kipindi hiki cha Kwaresima kwa ajili ya kuliombea taifa na dunia kwa ujumla. Na sasa tunafunga tena, hivyo kwangu jambo hilo ni majibu ya maombi tunayofanya. Nimefurahia kwa sababu naona maombi yanafanya kazi. Haya ni majibu, tunasema tumepita mashetani,”alisema Mama Maria huku akitania kuwa karne hii ni ya kisasa kweli, hata marehemu anaongea.
MWANANCHI
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amezuia uingizaji wa mabehewa 124 ya mizigo yaliyobaki katika zabuni iliyofanywa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), hadi pale uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika manunuzi hayo utakapokamilika.
Pamoja na hayo, Sitta alisema kuna hisia zimejitokeza kuwa huenda mabehewa hayo ni mitumba siyo mapya kama inavyodhaniwa.
Sitta aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa zabuni ilihusisha ununuzi wa mabehewa 274 na kwamba 150 tayari yalishaingia nchini, huku kukiwa na harufu ya ufisadi kuwa yalitengenezwa chini ya kiwango.
Mapema Aprili 2013, TRL iliipatia kampuni ya India iitwayo M/S Hindustan Engineering & Industrial Limited zabuni ya kutengenezea mabehewa ya mizigo kwa ajili ya Reli ya Kati. Serikali iliilipa kampuni hiyo Sh45.5 bilioni sawa na Sh166 milioni kwa kila behewa.
Hata hivyo, Sitta alisema kuwa Serikali ililipa asilimia 50 ya gharama zote za manunuzi na kwamba iwapo ikibainika udanganyifu wowote kampuni hiyo itawajibika.
“Nimekataza kabisa yale 124 yaliyobaki kule yasije. Nimeshawaagiza Reli kuwa yaliyopo kiwandani yanaendelea kutengenezwa au safarini hayaruhusiwi kuja kwa sasa mpaka tuweze kukwamua sakata hili.”
“Haiwezekani wakati tunachunguza 150 yaliyoingia tukayaruhusu yale 124 yaingie. Je, yakiwa na ubovu ule ule itakuwaje?” alihoji Sitta.
Alisema anaungana na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa mabehewa hayo ya mizigo yapo chini ya kiwango kutokana na kupinduka na kuacha reli mara kwa mara.
NIPASHE
Baraza la Maadili limeombwa kupendekeza kwa mamlaka inayohusika adhabu kali dhidi ya Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Ghulamhussein Dewji, kwa tuhuma za kumiliki mali mbalimbali, zikiwamo pikipiki 422 bila kuzitolea tamko katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mali nyingine ambazo Dewji anatuhumiwa kuzimiliki bila kuzitolea tamko katika sekretarieti hiyo, ni viwanja vitano; vinne kati yake, vikiwa katika eneo la Ipuli na kimoja Isule pamoja na nyumba moja yenye thamani ya Sh. milioni 16 iliyokuwapo katika eneo la Kazehili, katika manispaa hiyo.
Ombi hilo liliwasilishwa na Wakili wa Sekretarieti hiyo, Getrude Cyriacus, wakati akihitimisha hoja za upande wa malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma yaliyowasilishwa katika baraza hilo dhidi ya Dewji, wiki chache zilizopita.
Hata hivyo, Dewji (46), ambaye pia ni Diwani wa kata ya Kanyenye katika manispaa hiyo, ameliomba baraza limtendee haki, lisimuumize, limuonee huruma kwa madai kwamba hajakiuka popote, hivyo lione kuwa anataka kukandamizwa kwa chuki za kisiasa.
Wakili Getrude aliwasilisha ombi hilo baada ya baraza hilo linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Hamis Msumi, kusikiliza ushahidi wa uliotolewa na mashahidi wa pande zote mbili pamoja na utetezi wa mlalamikiwa, Ghulamhussein, katika baraza jana.
Wakili Getrude alidai ushahidi wa uchunguzi pamoja na nyaraka za vielelezo vilivyowasilishwa katika baraza na upande wa malalamiko unaonyesha kuwa pikipiki hizo bado ziko katika umiliki wa mlalamikiwa.
Hata hivyo, alidai pikipiki hizo zikiwa ni mali yake pamoja na viwanja na nyumba hiyo, mlalamikiwa hakuvitamka katika fomu yake ya rasilimali na madeni ya sekretarieti hiyo, kama Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inavyotaka.
Alidai zaidi ya hivyo, mlalamikiwa aliwahi kuitwa kuhudhuria Baraza la Maadili mkoani Tabora kwa barua, lakini hakuitikia wito huo.
Pia alidai mali alizonazo mlalamikiwa, yakiwamo magari matatu na duka moja, bado zimeandikwa jina lake na kwamba, sheria iko wazi na kwa hiyo, hawezi kutumia madaraka yake vibaya.
NIPASHE
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza rasmi kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwa madai ya kukiuka katiba ya chama hicho kutokana na kukishtaki mahakamani.
Uamuzi wa Chadema umechukuliwa baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Saalam jana kutengua pingamizi lililowekwa na Zitto katika kesi aliyoifungua mahakamani kuzuia kujadiliwa na Kamati Kuu ya Chadema hadi kesi yake ya msingi itakapomalizika.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema Zitto alikiuka katiba ya chama hicho kifungu cha 8(a)(X) ya kukipeleka mahakamani.
Alisema matatizo ya wanachama yatashughulikiwa kwa mujibu wa maadili na nidhamu yaliyopo ndani ya katiba ya chama hicho.
Lissu alisema pamoja na katiba ya chama kueleza utaratibu, lakini katika hali ya kushangaza, Zitto alikwenda mahakamani kukishtaki chama huku akifahamu wazi kuwa endapo atashindwa atakuwa amefukuzwa uanachama.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema kifungu cha 8(a)(X), mwanachama yeyote anapofungua kesi mahakamani dhidi ya chama, endapo atashindwa atakuwa amejiondoa uanachama,” Lissu.
“Zitto `ali-risk’ mwenyewe kukipeleka chama mahakamani huku akifahamu wazi kuwa endapo akishindwa atakuwa siyo mwanachama tena, alishauriwa vibaya ili akiharibu chama badala yake kimezidi kuimarika kuliko kilivyokuwa awali, matokeo yake tumemshinda na hicho kifo kilichotabiriwa hatujakiona, tumezidi kuwa imara kuliko ilivyokuwa awali,” alisema.
Aliongeza kuwa mahusiano kati ya chama na Zitto yalivunjika siku nyingi na walichokuwa wanasubiri ni uamuzi wa mahakama tu.
“Sisi hatuwezi kukubali kuwa na akina Yuda Eskarioti ndani ya chama chetu, taratibu zinazotakiwa kufanywa na chama hivi sasa ni kuiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili iwasiliane na mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema.
Alisema hatua nyingine itakayofuata mahakama itajulishwa kwamba Zitto si mwanachama tena kulingana na katiba ya chama hicho.
Lissu alisema baada ya mahakama kutoa uamuzi wa kesi aliyoifunga Zitto, Kamati Kuu ya Chadema haina haja ya kukaa na kujadili tena suala lake, isipokuwa Mahakama itatake notisi kuwa siyo mwanachama tena.
Kutokana na hali hiyo, Zitto jana alinukuliwa katika mitandao ya kijamii (facebook na Twitter) akisema hajui lolote kuhusiana na uamuzi uliofikiwa na mahakama na hakuwa na wito kuitwa mahakamani jana.
Alisema Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo amehamishiwa mkoani Tabora na hivyo hakuwa na taarifa ya jaji mpya aliyepangiwa kuendesha kesi hiyo.
“Kwa kesi ya Tegeta Escrow ilivyokuwa ingeshangaza waathirika kukaa bila kunivuruga, bahati mbaya sana sivurugiki ni kazi tu, mwanasheria wangu atatoa taarifa,” aliandika Zitto katika mitandao ya kijamii.
NIPASHE
Siku chache baada ya kifo na maziko ya aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), Kapteni John Komba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amemlilia akieleza kuwa ni mtu ambaye alikuwa ‘muumini asiyeyumba wa safari ya matumaini.’
Marehemu Komba ambaye alizikwa Jumanne iliyopita kijijini kwake Lituhi, anatajwa kuwa alikuwa rafiki wa karibu na Lowassa.
Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, alisema moyo wake unabubujika machozi ya damu kwa kuwa marehemu Komba alimshawishi agombee urais na amefariki dunia kabla hajampa jibu la kukubali au kukataa.
Alisema Kapteni Komba alikuwa mmoja wa makamanda wa kuongoza harakati za kumshawishi ajitose kwenye kinyang’anyiro cha urais.
“Ulipaza sauti bila woga kuelezea imani yako kwangu. Kapteni naumia sana umeondoka bila ya kukupa jibu la kukubaliana na ushawishi wako au la…kwa hakika Chama kimepata pigo.”
“Hivi ni kweli sitasikia tena sauti yako Kapteni Komba! Mbona umeondoka bila ya kuniaga ndugu yangu! Moyo wangu unabubujika machozi ya damu,” alisema Lowassa katika taarifa hiyo.
Alisema siku tatu kabla ya Komba kukutwa na umauti, alimtumia ujumbe kupitia kwa wasaidizi wake akimwambia ‘Mwambie Edward akija aje kuniona mimi sijisikii vizuri.’
“Maneno yako kwa mmoja wa wasaidizi wangu siku tatu kabla ya umauti kukupata, yanazunguka akilini mwangu…Kapteni Komba, mimi na wewe tumepigana vita nyingi kwa maslahi ya Chama na nchi yetu na tulishinda vita hivyo. Lakini bado tulikuwa tunaendelea na mapambano ya kumnasua Mtanzania katika umaskini,” Lowassa.
Aliongeza: “Ni nani asiyejua mchango wako katika ushindi wa chama chetu katika ngazi zote. Nyimbo zako ndiyo adhana au kengele ya kuwakusanya waumini (wana-CCM na wananchi), katika mikutano ya Chama. Komba ulikuwa nembo ya chama chetu.”
Alisema Komba ameondoka, lakini ameacha alama katika ulimwengu wa siasa hususan katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika taarifa hiyo, Lowassa alisema kwa kuwa alishirikiana na Komba kwenye nyakati za matatizo na furaha, atashirikiana na Chama kuendeleza pale alipoachia kutatua matatizo ya familia.
Kapteni Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu na mara kadhaa Ofisi ya Bunge ilimpeleka India kwa matibabu. Pia alikuwa na tatizo la kisukari ambalo ndilo lililochukua maisha yake.
Hivi ni kweli sitosikia tena sauti yako Captain Komba! Mbona umeondoka bila ya kuniaga ndugu yangu! Moyo wangu unabubujika machozi ya damu.
Maneno yako kwa mmoja wa wasaidizi wangu siku tatu kabla ya umauti kukupata kwamba “mwambie Edward akija aje kuniona mimi sijisikii vizuri” yanazunguka akilini mwangu.
Captain Komba, mimi na wewe tumepigana vita nyingi kwa maslahi ya chama na nchi yetu… na tulishinda vita hivyo. Lakini bado tulikuwa tunaendelea na mapambano ya kumnasua Mtanzania katika umaskini.
NIPASHE
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amejitwisha zigo la kashfa ya ununuzi wa mabehewa feki yaliyonunuliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) baada ya kuahidi kutangaza hatua atakazozichukua dhidi ya wahusika bada ya kupewa taarifa wiki ijayo.
Alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kumaliza kikao kati yake na menejimenti ya TRL.
Sitta alisema mabehewa 150 ambayo ni kati ya 274 yaliyonunuliwa na TRL kwa kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited baadhi yamekuwa yakiacha reli na kuanguka kutokana na kutokuwa na ubora unaotakiwa.
Alisema kwa mujibu wa taarifa zilizopo mfano katika kipindi cha Disemba, mwaka jana wastani wa mabehewa hayo kuanguka imekuwa ni kila siku na hivyo kusababisha hasara kwa serikali kwa sababu yanasababisha uharibifu wa njia ya reli.
Waziri Sitta alisema kutokana na tatizo hilo amemwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya TRL kukamilisha taarifa yao na kumkabidhi Jumatatu ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.
Alisema hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja ni kuvunja mkataba na kampuni iliyoiuzia TRL mabehewa hayo, kumshitaki mmiliki wa kampuni hiyo na kuwajibisha watendaji wa TRL ambao walihusika katika mchakato wa ununuzi wa mabehewa hayo kwa sababu wameliingiza hasara taifa.
Alisema pamoja na tatizo hilo, Shirika la Reli Tanzania (TRL) limeendelea kuwa bora siku hadi siku kutokana na mapato kuzidi kuongezeka ambayo yamefikia wastani wa Dola za Marekani milioni 140 mwezi Disemba mwaka jana.
Aliongeza kuwa kufikia mwishoni mwa Julai mwaka huu, vichwa vya treni vitakuwa vimefikia 60 kati ya mahitaji ya vichwa 107 hali itakayosaidia kurejesha usafiri wa treni kila siku katika mikoa ya kati.
Mabehewa mapya 25 ya kubebea kokoto aina ya ‘Ballist Hopper Bogie’ (BHB),yaliingizwa nchini na kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited yenye thamani ya Sh. bilioni 4.316 kwa ajili ya uimarishaji wa reli ya kati.
NIPASHE
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeeleza kutoridhishwa na bei ya mafuta nchini na imeielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kushusha zaidi bei hizo.
Kaimu Mwenyekiti wa PAC, Ismail Aden Rage, alitoa maelekezo hayo kwa bodi ya Ewura jana na kueleza kuwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia imeendelea kushuka hivyo wananchi wanapaswa kupata unafuu wa huduma mbalimbali kwa Ewura kushusha zaidi bei.
“Mafuta yameendelea kushuka kwenye soko la dunia lakini hapa nchini hayajashuka sana. Tunawapongeza kwa juhudi mlizochukua, lakini kamati hairidhishwi na bei hizi,” Rage.
Akijibu maelekezo hayo ya kamati, Mwenyekiti wa Bodi ya Ewura, Simon Sayore, alisema wataifanyia kazi hoja hiyo.
Hata hivyo, alisema mafuta yaliyoshuka bei kwenye soko la dunia ni ghafi na kwamba kuna msururu wa gharama ikiwamo za kuyasafisha, kusafirisha, kodi hapa nchini na nyingine za mamlaka kama Ewura, Shirika la Viwango (TBS), bandari na Wakala wa Vipimo, hazijashuka hivyo ni vigumu kwa mafuta kushuka sana.
Aidha, PAC imeiagiza mamlaka hiyo kujenga ofisi zake yenyewe badala ya kuendelea kulipa Sh. 1.2 bilioni kwa mwaka kama kodi ya pango.
MTANZANIA
Muimbaji wa muziki wa Injili, Flora Mbasha amesema yupo tayari kurudiana na mume wake Emmanuel Mbasha, ikiwa atakwenda kumuangukia miguuni na kumuomba msamaha.
Flora alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake juu ya kesi ya ubakaji inayomkabili Mbasha ambayo inasikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
“Mbasha nimemsamehe siku nyingi na nipo tayari kuishi naye iwapo atakuja kuniangukia miguuni na kuniomba msamaha… lakini hili (ubakaji) ni suala la mahakama,” alisema.
Alipoulizwa baba halali wa mtoto wake wa kike aliyejifungua hivi karibuni, alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo hivi sasa.
“Siwezi kulizungumzia nikifanya hivyo nitakuwa simtendei haki mwanangu. Siwezi kubadili mitizamo ya watu jinsi wanavyotafakari kuhusu jambo hili,” alisema.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga alisema awali Flora alitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Flora Mjaya na kueleza alivyosimuliwa na binti huyo anayedai kubakwa na Mbasha.
Katuga alikuwa akitoa ufafanuzi huo kwa waandishi kwa vile kesi hiyo inasikilizwa katika mahakamani ya siri kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2003 sura ya 20 kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu ili kulinda haki ya binti huyo.
HABARILEO
Polisi mkoani Rukwa inawashikilia watu 17 wakiwemo waganga wa jadi 10 wakihusishwa na tukio la kikatili katika kijijini cha Kipeta , Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ambako mtoto mlemavu wa ngozi (albino), Baraka Cosmas (6) mwishoni mwa wiki alishambuliwa na kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana.
Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni watu saba ambao wanatuhumiwa kushiriki katika kumkata kiganja mtoto huyo mlemavu wa ngozi akiwemo baba yake, mzazi Cosmas Yoram (32).
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Ferdinand Rwegasira amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao kufuatia msako mkali uliofanyika katika vijiji vinne vya wilaya za Sumbawanga na Nkasi.
Aliwataja waliokamatwa pamoja na baba mzazi wa mtoto huyo kuwa ni pamoja na Mwendesha William (30), Masunga Bakari (50) na Ngolo Masingija (47) wote kutoka kijiji cha Kaoze .
Wengine ni Paschal Jason (40), David Kiyenze (45) na Mageta Shimba (46), wote wakazi wa kikiji cha Kipeta , Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga.
Kwa mujibu wa Rwegasira, katika msako huo pia walikamatwa waganga wapiga ramli chonganishi 10 akiwemo Sererino Kachingwe “Nakalango”(70), mkazi wa kijiji cha Miangalua wilayani humo ambaye pia alipatikana na bunduki aina ya Shot gun greener yenye namba G 73354 TZD,CAR 47478 ambayo anaimiliki isivyo halali .
“Mtuhumiwa huyu pia ni mganga wa kienyeji ambapo alikutwa na wanyama wawili aina ya Kalunguyeye wakiwa hai pamoja na dawa mbalimbali za miti shamba. Pia katika msako huo amekamatwa mganga mwingine wa kienyeji , Eliza Malongo mwenye umri wa miaka 36 mkazi wa kijiji cha Kamnyalila akiwa na nyara za Serikali, “ alieleza.
Aliongeza Eliza alikutwa na ngozi ya chui, wanyama wanne waliokaushwa aina ya Kalunguyeye na nywele zinazodhaniwa kuwa za binadamu pamoja na mfupa wa swala.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook