Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Salum Morcase amkamate Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Saad Mutunzi Ishabailu kwa kosa la kuhamisha Tsh. 213,748,085 kwa awamu nne kwa njia ya uhamisho wa ndani kwa kushirikiana na Watumishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.
“Mkamate huyo bwana sasa hivi aende Polisi akafunguliwe mashtaka, huyu ni wa kupeleka Mahakamani moja kwa moja, DPP aelezwe afungue jalada la mashtaka, wale wenzake tumewapeleka Mahakamani tayari sababu tulibaini walihusika na wizi kama huu kwenye Manispaa ya Kigoma mwaka jana.”
Ametoa agizo hilo leo jioni Jumanne, Februari 27, 2024 wakati akiongea na Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwenye kikao kilichofanyika katika kwenye Halmashauri hiyo Mkoani Mara.
Waziri Mkuu amefikia hatua hiyo baada ya kuwaeleza Watumishi na Madiwani mbinu wanazotumia Watumishi wachache wa baadhi ya Halmashauri ambao walikuwa wanashirikiana na Watumishi watatu wa kitengo cha Treasury Single Account (TSA) kuiba fedha za umma.