Abiria wasiopungua 40 wamenusurika kifo baada ya basi lenye namba za usajili T 746 DKU aina ya Higer mali ya kampuni ya Salvation walilokuwa wakisafiria kutoka Bukoba kwenda Mwanza kupata ajali katika Kijiji cha Ilemela wilayani Muleba mkoani Kagera.
Basi hilo linalofanya safari zake kutoka Wilayani Karagwe kwenda Mwanza lilipata ajali baada ya dereva kuhama njia na kupinduka na kusababisha basi hilo kuwaka moto wakati akikwepa basi lingine lililotokea gafla mbele yake ambalo lilitaka kulipita basi lililokuwa limelitangulia.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi amesema tofauti na kawaida basi hilo ambalo leo limeanzia safari yake mjini Bukoba kwenda Mwanza lilipofika katika makutano ya Kyamunyorwa ndipo lilipokutana na mabasi mawili yaliyokuwa yakitoka Dar es Saalam kwenda Bukoba yakifukuzana na kulisababishia ajali.
“Basi la kwanza linafanya safari zake kutoka Dar es Saalam -Bukoba ambalo limetambulika kwa namba za usajili T 589 AUA aina ya Scania mali ya kampuni ya Super Video na la pili T 331 DHB aina ya Higher nalo linafanya safari kutoka Dar es Saalam -Bukoba’ Kamanda Malimi
“Haya mabasi mawili yalikuwa yanaongozana yakitokea barabara ya Biharamulo kwenda Bukoba na basi lililokuwa mbele ni basi lenye namba T331 likifuatwa nyuma na basi namba T589 wakati basi lililopata ajali lilikuwa linatokea uelekeo wa tofauti wa kutoka Bukoba kuelekea Mwanza” Kamanda Malimi
“Dereva huyo alilazimika kuhama njia na kwenda pembeni zaidi ambapo basi lilimzidi nguvu na kuanguka upande wa kushoto na kusababisha ajali ya moto,” Kamanda Malimi.