Wakati Shirikisho la soka la Afrika CAF likiipa adhabu nchi ya Morocco kwa kushindwa kushiriki michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika mwakani baada ya kujitoa kwa madai ya kuhofia ugonjwa hatari wa Ebola,tayari Shirikisho hilo limepata nchi mbadala ambayo itakua mwenyeji mwakani.
Baada ya makubaliano ya pande zote mbili CAF imekubali kuipa nafasi ya uenyeji Guinea ya Ikweta kuandaa fainali za kombe la Afrika 2015 ikichukua nafasi ya Morocco iliyojitoa wiki iliyopita.
Awali Rais wa CAF Issa Hayatou alikuwa na majadiliano yenye manufaa na Rais wa nchi hiyo Obiang Nguema mjini Malabo kabla ya kufikia hatua ya kuikabidhi nchi yake dhamana hiyo.
Taarifa ya CAF iliyotolewa na kituo cha BBC SWAHILI imethibitisha leo ijumaa kuwa Guinea ya Ikweta mojawapo ya nchi ndogo barani Afrika imepewa jukumu la kuokoa jahazi la michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika mwakani,na itashiriki fainali hizo kama ilivyo kawaida ya mwenyeji.
Nchi hiyo yenye kutumia kihispaniola kama lugha ya Taifa iliandaa fainali za Afrika za mwaka 2012 kwa pamoja na jirani yake Gabon.
Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Januari 17- Februari 8 mwakani kwenye miji ya Bata, Ebebiyin, Mongomo na mji mkuu Malabo na ikumbukwe mwaka 2012 walitumia miji miwili tu ya Bata na Malabo.
Sherehe za kupanga ratiba ya mechi za fainali hizo itafanyika mji mkuu wa Malabo mnamo Desemba 3 mwaka huu.
Taarifa ya CAF imesema kuwa Shirikisho hilo linawashukuru watu wa Guinea ya Ikweta, Serikali pamoja na Rais Ngwema mwenyewe kwa utayari wao wa kuokoa mashindano hayo.
Morocco ilijitoa kaandaa fainali hizo baada ya kuomba CAF isogeze mbele mashindano kwa ajili ya hofu ya ugonjwa wa Ebola ambao umeenea kwenye nchi kadhaa za Afrika Magharibi ambazo kwa kawaida hupeleka timu nyingi Zaidi katika fainali za Afrika.
CAF ilikataa mpango huo kwa madai kuwa haijawahi kuahirisha wala kufuta fainali hizo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957 na Morocco walipewa hadi jumamosi iliyopita kuthibitisha utayari wao wa kuandaa mashindano hayo lakini walishindwa kufanya hivyo na CAF ikaamua kufanya mchakato wa kutafuta nchi ya kuokoa na hatimaye kupatikana.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook