Mkazi wa Katavi, Augustino Laurent (27) amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kuchana mabango ya wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakili wa Serikali, Lugano Mwasubila amedai mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Janet Musaroche kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Septemba 21,2020 katika eneo la Misunkumilo ndani ya Mkoa huo.
Mwasubila amedai mtu huyo ambaye ni mkazi wa Makanyagio, ametenda kosa hilo kinyume na Kifungu cha 105 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 iliyofanyiwa Marejeo mwaka 2015.
Amesema mtuhumiwa anajishughulisha na uendeshaji wa bodaboda, ambapo visivyo halali alichana vipande vipande bango lenye picha ya Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli.
Pia mtuhumiwa huyo alichana tangazo lenye picha ya Mgombea Ubunge Jimbo la Mpanda Mjini kupitia chama hicho, Sebastian Kapufi na Mgombea Udiwani wa chama hicho, Alfred Matondo.
Amesema mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo na kesi yake itatajwa tena Oktoba 13,2020. Mtuhumiwa alipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.