Afisa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Ezekiel Mayumba, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro kwa kosa la kughushi nyaraka, kumdanganya mwajiri na ubadhirifu wa Sh6.1 milioni za chanjo.
Pamoja na kifungo hicho, Mayumba anatakiwa kurejesha fedha hizo baada ya kumaliza kifungo chake.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Manyara, Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati leo Alhamisi Mei 20, 2021 amesema Mayumba amehukumiwa na hakimu Charles Owiso.
Makungu amesema Mayumba ametiwa hatiani kwa makosa ya ubadhirifu wa Sh6.1 milioni za chanjo, kughushi matumizi ya nyaraka na kumdanganya mwajiri.
Amesema awali, mawakili wa Takukuru, Martin Makani na Evaline Onditi walimfikisha Mayumba mahakamani na kudhibitisha kuwa mashtakiwa huyo alitenda makosa hayo.
Makungu ametoa wito kwa watumishi wa umma kujiepusha na ubadhirifu wa mali ya umma kwa kuridhika na ujira wa haki wanaolipwa na wajiri wao.