Afisa wa Palestina amedai kuwa Israel itawaachia huru wafungwa 39 leo kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokubaliwa na Hamas.
Kundi hilo litaundwa na wanawake 24 na wavulana 15 kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu au Jerusalem, kamishna wa Palestina anayeshughulikia wafungwa Qadura Fares aliliambia shirika la habari la Reuters.
Watakabidhiwa kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu katika jela ya kijeshi ya Ofer ya Israel karibu saa kumi jioni kwa saa za huko (saa 2 usiku saa za Uingereza).
Hilo lingeenda sanjari na mpango wa makabidhiano katika mpaka wa Gaza-Misri wa mateka 13 waliochukuliwa na Hamas.
“Baada ya Shirika la Msalaba Mwekundu kuwapokea wafungwa hao (Wapalestina), wale kutoka Jerusalem wataenda Yerusalemu na wale wa Ukingo wa Magharibi watakusanyika katika baraza la manispaa ya Betunia, ambako familia zao zitakuwa zikisubiri,” Bw Fares alisema.
Kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano, Israel inatazamiwa kuwaachilia jumla ya wafungwa 150 katika mapatano hayo ya siku nne badala ya mateka 50 wanaoshikiliwa huko Gaza.