Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) kimeitaka Marekani kutathmini upya angalizo lake la ngazi ya 3 la kutosafiri nchini Rwanda ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na kituo hicho imesema kuwa imeitaka rasmi Wizara ya Afya na Huduma za Kibinadamu ya Marekani (HHS) na kituo cha CDC cha Marekani kutathmini upya na kuondoa angalizo lake la kusafiri lililotolewa Oktoba 7, likiwataka raia wake kufikiria upya kusafiri nchini Rwanda.
Mkurugenzi mkuu wa Afrika CDC Jean Kaseya amefuatilia hatua zilizopigwa na Rwanda katika kudhibiti mlipuko huo. Amebainisha kuwa angalizo la usafiri limekuwa na athari kubwa katika sekta ya utalii na biashara nchini Rwanda, ambazo zote ni muhimu kwa uchumi wake.