Serikali ya Afrika Kusini imeendelea kutambua na kuuenzi mchango wa Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo na bara la Afrika kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Mhe. Candith Mashego-Dlamini wakati akichangia hoja katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri la SADC uliomalizika tarehe 11 Machi 2024 jioni jijini Luanda, Angola.
Akizungumza kwenye agenda ya Sanamu ya Hayati Mwl. Julius Nyerere iliyozinduliwa rasmi tarehe 18 Februari 2024 jijini Addis Ababa, Ethiopia, Mhe. Dlamini alieleza kuwa uzinduzi wa sanamu hiyo ni ishara muhimu ya kuenzi jitihada na mawazo yake ambayo yataendelea kukumbukwa daima.
Aidha, alieleza kuwa Tanzania kupitia Mwl. Nyerere iliweka bayana nia ya dhati na ya wazi ya kuzikomboa Nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Afrika Kusini ambapo katika mapambano hayo ilitoa usaidizi wa kisiasa, mawazo, vifaa, hifadhi kwa viongozi na wapiganaji wake ikiwemo African National Congress (ANC) na Pan-African National Congress hadi pale walipofanikisha upatikanaji wa Uhuru wa Afrika Kusini mwaka 1994.
Tanzania ndio ilikuwa kimbilio la kwanza kwa Afrika Kusini baada ya kutokea kwa mauaji maarufu ya “Sharpeville massacre” yaliyotokea tarehe 21 Machi, 1960. Hatua hii ikaongeza chachu ya Mwl. Nyerere kuendeleza juhudi za kupinga ubaguzi wa rangi na ukoloni kwa ujumla wake na hivyo kujidhatiti kufanikisha kupatikana kwa uhuru kamili wa Afrika nzima.
Jitihada hizo zilipelekea kuanzishwa kwa Muungano wa nchi za Afrika (OAU) mwaka 1963 na baadae kuitwa Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2002 pamoja na uanzishwaji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU jijini Dar es Salaam iliyotoa misaada ya kifedha na vifaa katika kuchagiza harakati za ukombozi wa nchi za bara la Afrika zilizokuwa chini ya utawala wa kikoloni wakati huo Mwl. Nyerere akiwa miongoni mwa walezi wake.