Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anasema ni suala la muda tu kabla ya kusaini mswada wa Bima ya Afya ya Kitaifa kuwa sheria.
Mswada huo wenye utata, uliopitishwa na wabunge mwaka jana, unalenga kutoa huduma ya afya kwa wote kwa Waafrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Cape Town siku ya Alhamisi, Ramaphosa hata hivyo hakutoa maelezo zaidi ni lini hili linaweza kutokea.
Vyama vya kisiasa na washikadau wengine wanapinga vikali mswada wa NHI na wametishia kupeleka serikali mahakamani iwapo utatiwa saini kuwa sheria.
Wanasema itasababisha kutowekeza katika sekta ya afya, ambapo mifumo ya kibinafsi na ya umma ipo sambamba, na kuharibu uchumi wa Afrika Kusini ambao tayari ni dhaifu.
Pia kuna wasiwasi kwamba utekelezaji wa mswada huo utadhoofishwa na rushwa iliyoenea na vikwazo vya bajeti ambavyo vinasababisha nchi kuhangaika kufadhili huduma za msingi.
Madaktari wa Chama cha Madaktari cha Afrika Kusini wanasema hawaamini kwamba mswada huo utafanikisha kile kilichopangwa kufanya.