Chama cha kisiasa cha Economic Freedom Fighters ambacho kinaongozwa na Julius Malema nchini Afrika Kusini, kimefanya maandamano nje ya ubalozi wa Israel katika mji mkuu, Pretoria.
Kiongozi wa chama Julius Malema kwa mara nyingine tena alitoa wito wa kufungwa kwa ubalozi huo baada ya kusema kuwa serikali ya Israel “haiheshimu ubinadamu”.
Malema pia aliwataka wauzaji reja reja nchini kuondoa bidhaa zinazozalishwa na Israel kwenye rafu zao kufikia mwisho wa Oktoba.
“Ikiwa hawataondoa bidhaa kutoka Israel, tutaziondoa wenyewe. Hatutaki bidhaa za Israel ziuzwe Afrika Kusini, hatutaki chakula kutoka kwa watu ambao wana damu ya watu wasio na hatia mikononi mwao,” Alisema Malema.
Chama tawala cha African National Congress (ANC) kilifanya maandamano kama hayo nje ya ubalozi wa Israel siku ya Ijumaa.
Naibu Katibu Mkuu wa ANC Nomvula Mokonyane alitoa wito kwa Waafrika Kusini kususia uagizaji bidhaa kutoka Israel kwa mshikamano na Wapalestina.
Bi Mokonyane pia alisisitiza wito wa Afrika Kusini wa kusitisha mapigano mara moja katika Mashariki ya Kati.
Wiki iliyopita, msemaji wa Umoja wa Wanawake wa ANC alijiuzulu, akishutumu chama hicho kwa kushindwa kuelewa “upande wa hadithi ya Wayahudi” katika mzozo wa Israel na Palestina.