Jumuiya ya waislamu Waahmadiyya nchini kwa kuipitia taasisi ya Humanity First imekabidhi mifuko 600 ya saruji kwa ajili ya ukarabati na Ujenzi wa nyumba za waathirika wa maafa ya mafuriko wilayani Hanang Mkoa wa Manyara.
Mwenyekiti wa Humanity First Tanzania Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry ambaye pia ni Amir na Mbashiri Mkuu nchini ametoa salamu za pole kwa waathirika na kwamba ni muhimu binadamu akasaidiwa na binadamu mwenzake.
Akitoa taarifa ya msaada huo Naibu Amir Sheikh Abid Mahmood alisema kwamba Humanity First Tanzania hutoa misaada inayohusu usalama wa chakula, matatizo ya afya na uchimbaji wa visima ambapo kwa Tanzania vimechimbwa visima zaidi ya mia Tano.
Akikabidhi msaada kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Geoffrey Kasekenya anabainisha kuwa misaada iliyotolewa imepitia shirika la Humanity First kitengo maalum kinachofanya kazi ya kuwahudumia wanadamu bila ubaguzi wa rangi, dini, ukabila na utaifa katika nchi 209 Duniani ikiwemo Afrika na kwamba inawatumikia watanzania kwa namna yoyote inayohitajika.
Naibu Waziri Kasekenya amepongeza undugu na mshikamano ulioonyeshwa katika kusaidia na kuwafariji waathirika wa maafa ya mafuriko.
“Hii ni kuunga mkono jitihada za serikali za kusaidia wenzetu waathirika wa maafa haya tunahakika hii ni faraja kubwa kwetu na kwa Rais wetu” Ameeleza Kasekenya.
Kwa upande wake Sheikh wa Ahmadiyya mikoani Arusha, Manyara na Kilimanjaro Sheikh Shahab Ahmad ameeleza jumuiya inajengwa katika msingi wa usawa, uadilifu na haki kwa wanadamu wote duniani ili waweze kufurahia maisha ya Amani na usalama.
“Tunawaombea kwa Mola wetu Mlezi awajaalie viongozi wa Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama waweze kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili kuwafariji na kuwasaidia waathirika wa maafa haya”Amesema Ahmad.