Mahakama ya Wilaya ya Iringa imemuhukumu kifungo cha maisha mara mbili Mzee Selemani Gwabuga maarufu Msabato, sambamba na kulipa fidia ya shilingi milioni 25, kulipa faini shilingi milion 5 na kuchapwa viboko 11 baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka Mtoto wa miaka 11 na kumuambukiza virusi vya UKIMWI.
Mahakama imesema Mzee Msabato mwenye umri wa miaka 78 alikuwa akiishi kitongoji cha Idodi , Isimani Mkoani Iringa na alikuwa jirani na Mtoto huyo na mara kadhaa alikuwa akihubiri Injili.
Hukumu imetolewa baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu ikiwemo la kubaka Mtoto mwenye umri wa miaka 11 na kumuambukiza virusi vya UKIMWI kwa makusudi huku akijua yeye ni Mwathirika na anatumia dawa za kufubaza UKIMWI (ARVs) na kosa la tatu ni kujaribu kubaka Mtoto huyo wa miaka 11 aliyekuwa akisoma darasa la tano hivyo kosa la kwanza amehukumiwa jela maisha na kosa la pili akahukumiwa tena jela maisha.
“Siku ya kwanza baaada ya kumbaka Mtoto alimpa shilingi 200 na kumuambia asiseme kwa Mtu yeyote na katika tukio jingine Mtuhumiwa alikutana na Mtoto huyo mtoni na alipojaribu kumlazimisha Mtoto huyo Mama wa Mtoto alitokea na Mzee alikimbia na taratibu za kumkamata zikafanyika”
Kesi hiyo imesimamiwa na Waendesha mashtaka wa Serikali Nashon Saimon pamoja na Balton Mayage na ilikuwa na Mashahidi wanne akiwemo Daktari aliyethibitisha Mtoto huyo alikuwa ameingiliwa na kuambukizwa UKIMWI.