Ajali mbaya wa treni iliyotokea katika mji wa mashariki wa Bhairab, Bangladesh umesababisha vifo vya takriban watu 17 na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa huku maafisa wakihofia kuwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka.
Tukio hilo lilitokea wakati treni ya mizigo ilipogongana na treni ya abiria iliyokuwa ikienda kinyume na hivyo kusababisha mabehewa mawili ya abiria kuacha njia.
Sadiqur Rahman, msimamizi wa serikali huko Bhairab, alithibitisha matokeo ya kusikitisha, akisema kuwa miili 17 imepatikana, na zaidi ya watu 100 walipata majeraha.
Pia alielezea wasiwasi wake kuwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka kwani waokoaji bado wanafanya kazi ya kutoa miili chini ya makocha waliopinduliwa.
Katika kukabiliana na maafa hayo, treni ya uokoaji yenye kreni iko njiani kuelekea eneo la ajali ili kusaidia juhudi za uokoaji. Wakazi wa eneo hilo na watu waliojitolea walikimbilia eneo la tukio, wengi wao wakilia, wakiwatafuta wapendwa wao na kutoa msaada.
Ajali iyo ilitokana na treni moja kuingia kwenye njia sawa na nyingine, kulingana na Rahman.