Shirika la Reli Tanzania (TRC) limethibitisha kutokea kwa ajali ambapo basi la abiria lenye namba T178 DVB mali ya kampuni ya Ally’s Star Bus limepata ajali baada ya kugonga kichwa cha treni chenye namba V951 9006 kilichokuwa kikitokea Stesheni ya Aghondi kuelekea Manyoni katika makutano ya reli na barabara eneo la Manyoni mkoani Singida mapema leo na kusababisha vifo vya Watu 13.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Jamila Mbarouk imesema “Ajali imehusisha basi la abiria lililokuwa likivuka njia ya reli eneo la Kilomita 587 Manyoni na kugonga kichwa cha treni na kusababisha Majeruhi 25 (Wanawake saba, Wanaume 18) pamoja naa vifo vya Watu 13 (Wanawake 6 na Wanaume 7).
“Shirika litaendelea kuutaarifu umma kadiri taarifa zinavyopatikana na linaendelea kuwasihi Madereva wa vyombo vya moto kufuata sheria na alama za usalama katika njia ya reli na barabarani zilizowekwa ili kuepusha ajali, Shirika linatoa pole kwa Ndugu wa Marehemu na Mwenyezi Mungu awape nafuu majeruhi waweze kuendelea na shughuli za kujenga Taifa”