Jeshi la Polisi nchini Kenya linamshikilia kijana mmoja mwenye umri wa miaka 23 kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo kuhusu homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
Elijah Kitonyo amekamatwa akiwa katika Kaunti ya Kitui baada ya kuchapisha taarifa inayoeleza kuwa serikali imeudanganya umma kuhusu kisa cha kwanza cha muathirika wa Ugonjwa wa COVID-19 aliyepatikana nchini humo.
Kupitia mtandao wa Twitter, Katonyo alisema kuwa mgonjwa huyo alitokea Rome, Italia na si Marekani kupitia London, kama ambavyo taarifa ya serikali ilieleza.
Katika taarifa yake, ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imesema kuwa Katonyo atashtakiwa kwa kosa la kusambaza taarifa zinazosababisha mshtuko kwa umma.
Mtu atakayetiwa hatiani kwa kosa la kukiuka sheria ya mitandao nchini Kenya anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 10 jela au faini ya hadi shilingi milioni 115.6 au vyote kwa pamoja.
Wakati akitangaza mkakati wa kukabiliana na ugonjwa huo Machi 15, 2020, Rais Uhuru Kenyatta amewaonya wananchi kutosambaza taarifa za uongo.