Mhudumu wa zamani wa chumba cha kuhifadhai maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Iten, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet nchini Kenya amekamatwa na maafisa wa polisi kwa tuhuma za kuharibu miili iliyohifadhiwa hospitalini humo.
Benson Kagari ambaye ni mhudumu wa zamani wa mochwari hiyo, anaripotiwa kuingia katika mochwari ya hospitali hiyo Jumatano, Oktoba 28,2020 usiku, bila kugunduliwa na mtu yeyote.
Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Taifa leo, Waziri wa Afya katika Jimbo hilo, Isaac Kamar amesema mshukiwa aliingia katika hifadhi hiyo kupitia kwa dirisha na kuelekea hadi eneo ambapo miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa.
Inadaiwa mshukiwa alikuwa akiingia hospitalini humo kuharibu miiili iliyokuwa imehifadhiwa, Kamar amesema mshukiwa alitimuliwa hospitalini humo kutokana na utovu wa nidhamu.
“Tulipokea ripoti kwamba kulikuwa na mtu aliyeingia kwenye mochari ambapo alikuwa akiharibu miili iliyohifadhiwa na kuibadilisha ili kuwachanganya wahudumu.Tulifika kwa haraka na kubaini kuwa ni mhudumu wa zamani aliyefutwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu” Kamar
Kulingana na Kamar, baada ya kupokea ripoti hiyo maafisa wa afya waliingia chumbani humo kwa haraka na kumfumania mshukiwa ambapo walimkamata na baadaye walimkabidhi kwa polisi ili kuchunguzwa.
Inasemekana kuwa mshukiwa alitumiwa na baadhi ya watu flani kuwaharibia jina wafanyakazi katika hospitali hiyo ili kuonekana watepetevu.