Leo Desemba 3, 2020 Wabunge wa Viti Maalumu watatu (CHADEMA) akiwemo Halima Mdee wamemtambulisha Wakili wao mpya atakayewatetea katika kesi yao ya mashtaka saba ikiwemo kufanya uharibifu wa geti la Segerea.
Mbali ya Mdee, wabunge wengine ni Ester Bulaya na Jesca Kishoa pamoja washtakiwa wenzao 24 ambao wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao walifika mahakamani kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali ambapo walimtambulisha
Emmanuel Vkandis kuwa Wakili wao, huku washtakiwa wengine 24 wakitetewa na wakili Peter Kibatala.
Awali washtakiwa hao wote walikuwa wakitetewa na Wakili Hekima Mwasipo.
Washtakiwa hao wanaotetewa na Kibatala ni, Boniface Jakobo, Patrick Assenga, Henry Kilewo,Yohana Kaunya,Kedmony Mhembo, Mshewa Karua, Khadija Mwago, Pendo Raphael maarufu kama Mwasomola na mkazi wa Bonyokwa, Cesilia Michael, Happy Abdalla; Stephen Kitomali na Paul Makali
Hata hivyo mahakama imeshindwa kuwasomea washtakiwa hao PH na badala yake imetoa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa wawili, Edgar Adelini, Reginald Masawe, ambao hawajafika mahakamani hapo leo bila taarifa yoyote.
Awali wakili wa Serikali Ester Martin alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali lakini washtakiwa wawili hawajafika hivyo wameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo hayo na pia wameomba hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hao.
Katika hatua nyingine, mdhamini wa mshtakiwa Kedmony Mhembo, Remigius Bafuluki amewasilisha ombi la kujiondoa kumdhamini mshtakiwa huyo, lakini Hakimu amemwambia atajitoa pale ambapo atapatikana mdhanimi mwingine na amemtaka mshtakiwa Mhembo kutafuta mdhamini mwingine.