Serikali imesema kuwa uzinduzi wa alama ya asali ya Tanzania uliofanyika leo Oktoba 04, 2024 mkoani Tabora utasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza soko la asali ya Tanzania katika soko la kimataifa katika nchi mbalimbali ikiwemo China, barani Ulaya na Amerika.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika Chuo cha Ufugaji Nyuki mkoani Tabora,Waziri wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Balozi Dk.Pindi Chana amesema kuwa uzinduzi wa nembo ya asali ni katika muendelezo wa jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya mazao yanayotokana na asali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (Enabel) na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) ambao wamewezesha mchakato wa kupatikana alama hii.
Akizungumza mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya wa Wilaya, Wakurugenzi na viongozi wengine waandamizi na wadau wa maendeleo, Balozi Chana amesema alama hii ina faida mbalimbali, ikiwemo kuitenganisha kwa ubora asali ya Tanzania na asali nyingine katika masoko ya ndani na nje na kuwahakikishia walaji (watumiaji) ubora wa asali hiyo.
Amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali katika kuhakikisha asali inaongeza pato la taifa na kuingiza pesa za kigeni kwa kuwainua wajasiriamali na wafanyabiashara wanaotengeneza vifaa vya kurina asali.
Amesema moja ya mikakati hiyo ni upatikanaji wa soko la asali nchini China uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassana wakati wa ziara yake nchini China hivi karibuni, akiwataka wafanyabishara kujiandikisha kwa wakala wa huduma za misitu ili kuanza kuchangamkia fursa hiyo.
“Kuna fursa nyingi sana, kwa sasa kama nchi tunazalisha tani 33276 tu za asali kwa mwaka, lakini uwezo wetu ni kuzalisha zaidi ya tani 138,000, hivyo, tuhimize watu kushiriki katika ufugaji nyuki ili kuongeza wigo zaidi wa biashara,”, amesema.
Amesema jitihada nyingine ni Serikali kushirikiana na wadau wa mradi huu ikiwemo EU ambayo imetoa bilioni 2.6 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wasichana katika chuo hicho cha Nyuki mkoani Tabora, ambapo Waziri Chana pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi huo wa ghorofa mbili lenye zaidi ya vyumba 37 kwa ajili ya takriban wanafunzi 148.
“Tunawashukuru sana wadau kwa kushirikiana na Serikali katika kusaidia ukuaji wa sekta ya asali hapa nchini kupitia mradi wa Kuongeza Thamani Mazao yanayotokana na Nyuki (BEVAC) ambao unatekelezwa Tanzania Bara na Visiwani,” amesema Waziri Chana.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Zanzibar Ally Hamis Juma amesema mradi huo umekuwa na tija pia visiwani Zanzibar, akiisifu Serikali na wadau ikiwemo EU, Enabel, International Trade Centre, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kwa utekelezaji wake.
Akimkaribisha Waziri Chana, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Martin amesema mkoa wake unachukua hatua mbalimbali ikiwemo kulinda misitu kwa ajili ya uzalishaji asali mkoani humo.
Akitoa maelezo kuhusu uanzishwaji wa alama hiyo, Meneja wa mradi wa BEVAC Stephen Paul amesema utengenezaji wa alama hiyo umepitia mchakato na kuhusisha taasisi mbalimbali ikiwemo Tantrade, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na lile la Zanzibar (ZBS) katika utengenezaji wake.
Akiongea katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Tantrade Crispin Luanda amesema alama hiyo itaipeperusha vema asali ya Tanzania kimataifa na kufanya vizuri kwa sababu masoko ya kimataifa yanaamini sana vilelezo muhimu ikiwemo alama kutoka nchi husika.
Naye Mwenyekiti wa bodi wa Chuo hicho cha Nyuki mkoani Tabora Dr. Angela Mwakatobe ameshukuru kwa ujenzi wa bweni la wasichana kupitia BEVAC ikiwa kama sehemu ya mkakati wa ukuzaji wa sekta ya mazao ya asali hapa nchini.
Pia wajasiriamali na wafanyabiashara walioshiriki maonesho ya bidhaa zitokanazo na asali chuoni hapa kabla ya uzinduzi wa alama hiyo wamesifu jitihada hizo zinalenga kuwakomboa kiuchumi.
Ashura Mwazembe kutoka kikundi cha Mzinga wa Mama Samia amesema kuwa wanategemewa kwenda katika maonesho ya Asali nchini Sudan Kusini na nembo hii itawabeba kufanya vizuri katika maonesho hayo kwa sababu asali ya Tanzania ni namba moja kwa viwango barani Afrika.