Algeria itafanya uchaguzi wa urais wake Septemba 7, na kumpa Rais Abdelmajid Tebboune zaidi ya miezi mitano kufanya kampeni iwapo ataamua kuwania muhula wa pili wa kuliongoza taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta kaskazini mwa Afrika.
Ofisi ya rais ilitangaza tarehe hiyo katika taarifa Alhamisi baada ya kukutana na kundi lililojumuisha wabunge wa ngazi za juu na mahakama ya kikatiba pamoja na halmashauri yake huru ya uchaguzi.
“Iliamuliwa kuandaa uchaguzi wa mapema wa rais mnamo Septemba 7, 2024,” imebainisha ofisi ya rais wa jamhuri katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mwishoni mwa mkutano ulioongozwa na mkuu wa nchi Abdelamadjid Tebboune, mbele ya Waziri Mkuu wake , wakuu wa Mabunge mawili, Mkuu wa Majeshi na Rais wa Mahakama ya Katiba.
“Baraza la uchaguzi litaitishwa mnamo Juni 8, 2024,” imeongeza taarifa kwa vyombo vya habari.
Uchaguzi uliopita wa urais, ambao Bw. Tebboune alishinda kwa asilimia 58 ya kura na kukumbwa na kiwango kidogo cha ushiriki , ulifanyika Desemba 12, 2019. Alimrithi Abdelaziz Bouteflika, ambaye alilazimika kujiuzulu mwaka wa 2019 kwa shinikizo kutoka kwa jeshi na Hirak, vuguvugu la kiraia la maandamano. Alifariki mnamo Septemba 2021.