Serikali ya Algeria imekataa kuruhusu ndege za kivita za Ufaransa kutumia anga yake kwa ajili ya kuelekea Niger na eneo la Sahel Afrika.
Redio rasmi ya Algeria imemnukuu afisa ambaye hakutaka jina lake litajwe akisema kwamba, serikali ya Algiers imekataa ombi la Ufaransa la kuruhusu ndege zake za kijeshi kutumia anga ya nchi hiyo kuelekea Niger kutokana na msimamo wa Algiers inayopinga uingiliaji wa kijeshi wa nchi za kigeni nchini Niger kwa kisingizio cha kurejesha utawala wa kikatiba.
Hivi karibuni, katika Mkutano wa 11 wa Kimataifa wa Usalama wa Moscow,Luteni Jenerali, Al-Saeed Shangriha, Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Algeria, alionya dhidi ya uingiliaji wowote wa kijeshi wa kigeni nchini Niger, ambao utasababisha ukosefu wa utulivu katika eneo la Sahel barani Afrika, na akatoa wito wa kurejeshwa utawala wa sheria na na utekelezaji wa katiba katika nchi hiyo bila uingiliaji wa nchi za kigeni.
Algeria, ambayo daima inapinga matumizi ya nguvu, imekataa ombi hilo la Ufaransa na jibu lake lilikuwa wazi na la moja kwa moja.
Jumapili iliyopita pia, Algeria ilieleza kuchukizwa kwake na uamuzi wa kundi la ECOWAS linaloungwa mkono na Ufaransa wa kutumia nguvu za jeshi kwa ajili ya kumrejesha madarakani kiongozi aliyepinduliwa nchini Niger na kueleza kwamba, inasikitishwa kuona kuwa matumizi ya nguvu za kijeshi yamepewa kipaumbele zaidi badala ya kutafuta suluhisho la kisiasa na mazungumzo kwa ajili ya kutatua mzozo nchini Niger.