Mkazi wa Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, Zacharia Samweli, maarufu kwa jina la Balozi (59) jana amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na kosa la kumbaka Binti wa miaka 14.
Akisoma hukumu hiyo Jumatano Machi 3, 2021, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga, Ushindi Swalo amesema amejiridhisha na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo pasipo shaka na kumtia hatiani mtuhumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30.
“Baadhi ya wanaume wamekuwa wakitenda makosa mengi ya kubaka wanawake na wengine hubaka watoto wadogo hili litakuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo,” Hakimu Swalo.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali Mkuu, Venance Mkonongo, akisaidiwa na Wampumbulya Shani alisema mhanga alianza kubakwa tangu Januari mwaka 2016 katika mtaa wa Mshikamano ambako wazazi wake wamepanga.
Inadaiwa kuwa wazazi wa mwathirika walikuwa wamepanga katika nyumba ya Zacharia Samweli (mshtakiwa) iliyoko katika mtaa wa Mshikamano Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga ambapo alianza kumrubuni binti huyo na kuanza kumbaka kwa nyakati tofauti kwa kipindi kirefu.
Kesi hiyo ya ubakaji ilifunguliwa Machi 5, mwaka 2020 na kutolewa hukumu Machi 3, mwaka huu, ambapo hatua hiyo ni jitihada na mwendelezo wa Serikali katika kupiga vita na kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.
MAPYA GENIUS WA HESABU APATA SHULE YA KISHUA “KURUSHWA DARASA NI KIBOKO, ANAWAZIDI DARASA LA SABA”