Mbunge wa zamani wa Malawi, Clement Chiwaya, amejiua mwenyewe kwa kujipiga risasi nje ya bunge.
Bwana Chiwaya, ambaye alikuwa akitumia kiti cha kusukuma tangu apate ugonjwa wa polio akiwa na umri wa miaka miwili, alikuwa naibu spika kati ya mwaka 2014 na 2019.
Katika ujumbe ambao aliuacha kabla hajaenda bungeni huko Lilongwe, aliandika kuhusu mgogoro aliokuwa nao kati yake na Bunge juu ya umiliki wa gari.
Baada ya kushindwa kwenye uchaguzi, alianza mchakato wa kutaka kununua gari ambalo alipewa na bunge lililomwezesha kuendesha licha ya ulemavu wake. Alilipia gari hilo lakini alilishutumu Bunge kwa kushindwa kumpa haki ya umiliki.
Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa aliingia ofisi ya maulizo ya Bunge siku ya AlhamisI na kujipiga risasi mwenyewe. Katika ujumbe aliouacha, alisema amechoka kuomba kwa kile ambacho ni chake na ameamua kujiua akihofia kuumiza wengine.
Bwana Chiwaya, alizaliwa mwaka 1971, akawa mwanaharakati wa haki za walemavu na kufanikiwa kuwa Mbunge mara tatu. Polisi wanachunguza sasa ni namna gani aliweza kuingia bungeni, eneo ambalo lina ulinzi mkali.