Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Mkuu wa zamani wa majeshi nchini Burkina Faso, Luteni Kanali Évrard Somda, ametekwa nyara na “watu wenye silaha” akiwa nyumbani kwake katika mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou.
Chanzo cha usalama kilicho karibu na afisa huyo kimesema,”alitekwa nyara jana (Jumapili) akiwa nyumbani kwake na watu waliokuwa na silaha: walizingira eneo alikokuwa akiishi, wakaizingira nyumba yake kabla ya kumkamata”.
“Haijulikani kama alikamatwa kwa amri ya jeshi au mahakama, au kama ni utekaji nyara mwingine,” kimesema chanzo kingine kilicho karibu na mkuu huyo wa zamani wa jeshi, kikithibitisha habari hiyo. Chanzo hicho kimeeleza kwamba “hakuonyesha upinzani wowote” na “aliwafuata watu waliokuja kumchukua na kumpeleka kusikojulikana”.
Akiwa ameachishwa kazi mwezi Oktoba baada ya kukamatwa kwa maafisa wanne, wakiwemo wawili waliokuwa washirika wake wa karibu walioshukiwa kuhusika katika “njama ya kuhatarisha usalama wa taifa”, kitendo ambacho utawala wa kijeshi ulioko madarakani ulidai kuzima, Luteni Kanali Evrard Somda hakuwa anaondoka nyumbani kwake, kulingana na ndugu zake.