Mwanamke aliyesema kuwa ni haki kumuua mwanaume aliyekua akimsafirisha na kwenda kumuuza kingono amehukumiwa kifungo cha miaka 11 jela Jumatatu wiki hii baada ya kukiri makosa ya kufanya mauaji kizembe.
Jaji wa kaunti ya Kenosha, Wisconsin USA, amemhukumu Bi. Chrystul Kizer miaka 11 ya kifungo cha awali ikifuatiwa na miaka 5 ya uangalizi baada ya kuhusika katika kifo cha Randall Volar, 34 kilichotokea mwaka 2018.
Kizer alikiri kosa la mauaji daraja la pili mwezi Mei mwaka huu ili kumruhusu kukwepa kesi na uwezekano wa kifungo cha maisha jela, waendesha mashtaka walisema alimpiga risasi Volar nyumbani kwake, alipokuwa na umri wa miaka 17, kisha akachoma nyumba yake na kuiba gari aina ya BMW.
Mwanamke huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 24, alisema alikutana na Volar kwenye tovuti ya biashara ya ngono, alikuwa akimnyanyasa na kumuuza kama kahaba kwa mwaka mmoja hadi kifo chake, aliwaambia wapelelezi kwamba alimpiga risasi baada ya Volar kujaribu kumshika.