Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limesema kuwa waandamanaji kadhaa wanaopinga ukatili unaotekelezwa na Polisi mjini Lagos nchini Nigeria wameuwawa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, shirika hilo la kimataifa la Amnesty International limefahamisha kuwa polisi walilazimika kutumia risasi za moto na vitoa machozi kuwatawanya zaidi ya waandamanaji elfu moja waliokuwa wamekusanyika katika mji wa kibiashara wa Lagos, nchini Nigeria.
Shirika hilo linasema waandamanaji kadhaa walipoteza maisha na maelfu ya wengine walijeruhiwa kwa kupigwa risasi, kwa mujibu wa mashuhuda.
Maandamano zaidi yameshuhudiwa kote nchini Nigeria kupinga kikosi maalum cha polisi cha kukabiliana na wizi (SARS) kikilaumiwa kwa kuendesha vitendo vya kikatili nchini humo.