Raia mmoja katika Wilaya ya Kalaki nchini Uganda (35), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kumnyonga hadi kufa mwanaye mwenye umri wa miezi tisa baada ya kukosa kupokea msaada wa Sh. 100,000 kwa watu wasiojiweza wa kujikidhi katika kipindi cha tahadhari ya corona.
Hivi karibuni Serikali ya nchi hiyo iliahidi kutoa Sh 100,000 kwa watu wasiojiweza ili kuweza kujikimu kwa kipindi cha siku 42 ambacho walipaswa kukaa ndani ikiwa ni moja ya hatua za kujikinga na maambukizi ya corona.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkuu wa wilaya hiyo, Paul Kalikwani mtuhumiwa aliposikia baadhi ya watu wamepokea kiasi hicho cha fedha kwenye simu zao lakini kwake hakuwa amepata ujumbe wowote aliamua kufanya maamuzi hayo ya kumyonga mtoto wake.
Awali mtuhumiwa huyo alishawahi kusikika akiwaambia wanakijiji wenzake kuwa iwapo serikali haitampatia fedha hizo ataua familia yake yote.