Amri ya kutotoka nje imewekwa katika jimbo la pili kwa ukubwa nchini Nigeria, Kano, baada ya maandamano ya kupinga gharama kubwa ya maisha “kutekwa nyara na majambazi” ambao walijihusisha na uporaji na uharibifu wa mali, ofisi ya gavana imesema.
Kano aliona umati mkubwa zaidi katika siku ya kwanza ya maandamano ya kitaifa ambayo yalilazimu biashara nyingi kufungwa.
Waandamanaji katika majiji yote makubwa waliingia barabarani, wakiimba kauli mbiu kama vile: “Tuna njaa.”
Polisi walifyatua risasi za moto na gesi ya kutoa machozi – na kunyunyiza maji ya moto – kujaribu kuwatawanya maelfu ya waandamanaji katika jiji la Kano.
Watu wanne walijeruhiwa, na kupelekwa hospitalini.
Amri ya kutotoka nje inazuia maandamano kuendelea, huku wakaazi wote wakitarajiwa kusalia nyumbani.
Sensa ya mwisho nchini Nigeria, mwaka 2006, iliweka wakazi wa jimbo la Kano kufikia milioni 9.4, huku makadirio yasiyo rasmi yakiweka idadi ya sasa ya watu kuwa karibu milioni 20.
Maandamano hayo – yaliyoitishwa kwa siku 10 – yameandaliwa kupitia mitandao ya kijamii na kuchochewa na mafanikio ya hivi majuzi ya waandamanaji nchini Kenya ambao walilazimisha serikali kufuta mipango ya kuongeza ushuru.