Mteja mmoja wa Pizza aitwae Charles Leggett (38) amempiga risasi na kumuua Muhudumu wa Mgahawa wa Pizza huko Milwaukee Nchini Marekani aitwae Jamil Owais (26) katika ugomvi ambao umetokana na Charles kusema Mpishi hakuwa amevaa gloves mikononi wakati wa kuiandaa pizza hiyo
Jamil Owais alikuwa akifanya kazi katika Mgahawa wa Familia uitwao Action Food & Liquor ambapo kwa mujibu wa Kaka yake aitwae Mohammad Owais, Marehemu alipigwa risasi ya kifua na kufariki.
Charles ambaye tayari amekamatwa na Polisi akikabiliwa na kifungo cha miaka 75 iwapo atapatikana na hatia, ana rekodi ya makosa ya jinai Nchini humo na wakati tukio hili linatokea alikuwa ameshapigwa marufuku ya kumiliki silaha.
Hata hivyo Mpishi aliyeandaa pizza hiyo alithibitisha kwamba alikuwa amevaa gloves wakati wa maandalizi hivyo mzozo huo haukuwa na maana yoyote na umesababisha kifo cha Jamil na kuiachia Jamii yake huzuni kubwa kwani alikuwa Mtu mkarimu na aliyeheshimu kila Mtu katika Jamii yake.