Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye ameliagiza Jeshi la Polisi Kigoma kumkamata na kumfutia dhamana mwanaume anaekadiriwa kuwa na umri wa miaka sitini anaetuhumiwa kumlawiti mwanafunzi wa darasa la nne mwenye umri wa miaka kumi na mbili.
Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari waliofika Ofisini kwake kwa lengo la kumtaka aingilie katika kuona namna kukomesha vitendo vya ulawiti, ubakaji na matukio mengine ya ukatili hususani kwa wanawake na watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa na kuishia hewani.
Tukio la kulawitiwa kwa Mwanafunzi huyo ambaye ambae jina lake limehifadhiwa limetokea September mwaka huu tarehe ambayo haikutajwa na kuripotiwa Kituo cha Polisi Central Mjini Kigoma October 26.
Aidha sababu za kuchelewa kuripotiwa kwa tukio hilo zinaelezwa kuwa ni baada ya Mtuhumiwa ambaye ni Mjomba wa Mwanafunzi huyo kumwambia atakatisha maisha yake ikiwa atatoa taarifa kwa mtu yeyote hali iliyopelekea Mtoto huyo kushindwa kutoa taarifa kwa wakati huku akiendelea kusumbuliwa na maradhi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Alchelaus Mutalemwa amekiri kuripotiwa kwa tukio hilo na kuahidi kufanyia kazi agizo la RC haraka iwezekanavyo ili kuona haki ya mwanafunzi huyo ambae anahangaika kupata matibabu ili arejee shuleni kuungana na wenzake katika Mtihani wa Taifa wa darasa la nne mwaka huu inatendeka.
Kwa sasa tayari Polisi wamefanikiwa kumtia nguvuni mtuhumiwa wa tukio hilo.