Kipa André Onana huenda akajumuishwa katika kikosi cha Cameroon kwa ajili ya mchezo wa makundi wa Kombe la Mataifa ya Afrika Ijumaa dhidi ya mabingwa watetezi Senegal baada ya kurejea mazoezini na timu hiyo Jumatano.
Onana alikosa mechi ya ufunguzi ya Cameroon ya michuano hiyo nchini Ivory Coast Jumatatu baada ya kuruhusiwa kusalia Manchester United na kucheza katika sare ya 2-2 na Tottenham Hotspur siku ya Jumapili.
Alisafiri kwa ndege ya kukodi usiku kucha hadi Ivory Coast baada ya mpambano huo uliochezwa Old Trafford lakini alifika saa chache tu kabla ya kuanza kwa mpambano wa Kundi C dhidi ya Guinea, ambapo Cameroon walitoka nyuma na kulazimisha sare ya 1-1.
Uamuzi wa kumruhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 kuacha mechi ya ufunguzi wa michuano hiyo ulizua utata miongoni mwa wafuasi wa Cameroon.
Katika mahojiano baada ya kuwasili Ivory Coast, Onana aliwaambia waandishi wa habari juu ya mvutano mgumu wa uaminifu kati ya klabu na nchi, haswa kwa wachezaji wa kimataifa wa Kiafrika waliolazimika kuzihama vilabu vyao vya Ulaya katikati ya msimu ili kushiriki Kombe la Mataifa.
“Ni sawa na kuchagua kati ya baba na mama yangu, lakini nchi yangu inatangulia, ndiyo maana nipo hapa,” alisema.
“Wacha watu waendelee kunikosoa. Nimezoea. Ninafanya kile ambacho ni cha manufaa kwa nchi yangu,” Onana aliongeza.