Andreas Brehme, mfungaji wa bao la ushindi la Ujerumani katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1990, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 63.
Beki huyo wa kushoto alifunga mkwaju wa penalti dakika ya 85 huku vijana wa Franz Beckenbauer wakiilaza Argentina 1-0 mjini Rome.
Brehme aliichezea Ujerumani mara 86 na pia alishinda Bundesliga akiwa na Kaiserslautern na Bayern Munich, pamoja na taji la Serie A akiwa na Inter Milan.
Bayern walitoa heshima kwa mchezaji wao wa zamani, wakisema: “FC Bayern wamehuzunishwa sana na kifo cha ghafla cha Andreas Brehme. Tunatoa pole nyingi kwa familia yake na marafiki.
“Andreas Brehme atakuwa daima mioyoni mwetu, kama mshindi wa Kombe la Dunia na, muhimu zaidi, kama mtu wa pekee sana. Atakuwa sehemu ya familia ya FC Bayern milele. Pumzika kwa amani, Andi!”