Umati wenye hasira nchini Pakistan ulimtuhumu mwanamke aliyevalia vazi lililopambwa kwa maandishi ya Kiarabu kwa kukufuru, baada ya kuwakosea kwa aya za Quran.
Aliokolewa na polisi waliomsindikiza hadi mahali salama baada ya mamia kukusanyika.Baadaye aliomba msamaha kwa umma.
Nguo hiyo ina neno “Halwa” lililochapishwa kwa herufi za Kiarabu juu yake, likimaanisha tamu kwa Kiarabu.
Kukufuru kunaadhibiwa na kifo nchini Pakistan. Baadhi ya watu wamehukumiwa hata kabla ya kesi zao kuanza kusikilizwa.
Polisi waliambia BBC kwamba walipokea simu kwa mara ya kwanza mwendo wa saa saba unusu kwa saa za eneo (08:10 GMT) siku ya Jumapili kwamba umati ulikuwa umemzunguka mwanamke katika mgahawa huko Lahore, mji mkuu wa jimbo la Pakistani la Punjab.
Takriban watu 300 walikuwa wamejazana nje ya mgahawa huo walipofika, alisema Mratibu Msaidizi Syeda Shehrbano.
Video za tukio hilo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, huku moja ikimuonyesha mwanamke, akionekana kuwa na hofu, akiwa ameketi pembeni kabisa ya mgahawa huo, akiukinga uso wake kwa mkono wake.
Katika video nyingine alionekana amezungukwa na maafisa, ambao walikuwa wameweka kizuizi pekee kati yake na umati uliokua ukiongezeka na walikuwa wakipiga kelele wakimtaka avue shati.