Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi inayomkabili Mhasibu Mkuu wa (TAKUKURU), Godfrey Gugai anayedaiwa kumiliki mali zenye thamani ya sh. Bilioni tatu ambazo haziendani na kipato chake hadi January 2,2018 kwa sabau upelelezi haujakamilika.
Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, kuwa shauri limeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.
Kutokana na kutokamilika kwa upelelezi huo, Wakili Peter aliomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa aliomba upande wa Jamhuri watoe maelezo ambayo yataeleza lini upelelezi utakamilika ambapo upande wao utajua siku ya kuanza kwa usikilizwaji wa shauri hilo.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Peter alidai kukamilika kwa upelelezi ni hatua, hivyo hawawezi kueleza kwa asilimia ngapi ila bado unaendelea na wako katika hatua nzuri.
Wakili huyo alidai tarehe ijayo wataeleza hatua ya upelelezi ilipofikiwa.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote husika, Hakimu Simba aliahirisha shauri hilo hadi January 2, 2018 kwa kutajwa na washitakiwa walirudishwa mahabusu.
Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera
Washitakiwa hao wanaokabiliwa na mashitaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.
Katika mashitaka hayo, shitaka la kwanza ni la kumiliki mali ambazo hazina maelezo ambalo linamkabili Gugai anayedaiwa kati ya January 2005 na December 2015, mkoa wa Dar es Salaam, akiwa ofisa wa umma ameajiriwa na TAKUKURU anamiliki mali zenye thamani zaidi ya sh. bilioni tatu ambazo haziendani na kipato chake cha sasa wala cha nyuma cha sh. milioni mia nane.
MAHAKAMA KUU YA TANZANIA IMEMUACHIA HURU SHEIKH ISSA PONDA, BONYEZA PLAY HAPA CHINI KUTAZAMA