Mke wa Kigogo wa Kampuni ya Usafirishaji wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam(UDART), Robert Kisena, Frolencia Membe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka saba ikiwamo uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha zaidi ya Bilioni 2.4.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwizile, Wakili wa Serikali, Ester Martin amedai mshitakiwa huyo ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta na Gesi ya Zenon alitenda makosa hayo katika nyakati tofauti kati ya mwaka 2011 hadi 2018.
Katika mashitaka hayo inadaiwa mshitakiwa aliratibu shughuli za uhalifu katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2017. Pia anadaiwa kujenga kituo cha mafuta cha Petroleum Filling Station kati ya Januari 2015 hadi Desemba 31,2017 katika eneo la Jangwani,Ilala Jijini Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiri wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Kosa jingine anadaiwa kati ya Januari 25,2015 hadi Desemba 2017, akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Zenon na wenzake, wanadaiwa kufanya biashara ya kuuza mafuta katika eneo lisiloruhusiwa la Jangwani kinyume na sheria ya mafuta.
Pia katika tarehe hizo kati ya Januari 25,2015 hadi Desemba 31,2016, mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi anadaiwa kuiibia Kampuni ya usafiri ya Mabasi Yaendayo Kazi Mkoa wa Dar es Salaam(Udart) mafuta yenye thamani ya Sh bilioni 1.2.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, mtuhumiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana, pia upelelezi wa kesi huyo bado unaendelea. Kesi imeahirishwa Aprili 23, 2019.