Wakati gumzo la mkataba wa uwekezaji Bandarini Dar es salaam likiendelea, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa ameongea leo na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam na kuelezea mengi ikiwemo hoja za kisheria ambazo amedai baadhi ya Wanasheria wanaozijadili aidha hawazijui au wanafanya makusudi.
“Ukiwasikiliza wengi Mtu anaweza kuongea kwa dakika 15 lakini hakuna sehemu yoyote anafika kuzungumzia yale makubaliano yenyewe yaliyoingia kati ya Serikali yetu na Serikali ya Dubai na wanafanya hivyo kwa makusudi kwasababu yapo maneno mengi ambayo unaweza kuongea na ukatengeneza sintofahamu na taharuki”
“Zipo hoja za kisheria ambazo na zenyewe ninasikitishwa baadhi ya Wanasheria kuzijadili katika mrengo ambao aidha hawazifahamu au wanafanya makusudi, kwa mfano IGA ni makubaliano ya Kimataifa”
“IGA ukiisoma hakuna eneo lolote bandari inaenda kubinafsishwa, IGA inaenda kujenga msingi wa kwenda kuingia kwenye mkataba wa uendeshaji, swali ni je hii ni mara ya kwanza?, leo ukienda Uwanja wa Ndege wa Mwl Nyerere unamilikiwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege lakini ukienda kuangalia operesheni za uwanja zinafanywa na Sekta binafsi”
“Swali linakuja je pale Airport masuala ya ulinzi na usalama yanasimamiwa na nani?, yanasimamiwa na Serikali chini ya Vyombo vyetu pale kuna Kituo cha Polisi , je kodi inakusanywa na nani pale Airport?, inakusanywa na TRA”