Bunge la Kenya limepiga marufuku uvaaji wa kaunda suti ndani ya Bunge ambapo Spika wa Bunge, Moses Wetangula, amesema suti hizo pamoja na nguo za asili ya Afrika, hazikubaliki na hii ni kutokana na mitindo mbalimbali ya ushonaji wa suti hizo ambayo inakiuka kanuni za mavazi ya Bunge.
Vazi hilo la suti lililopewa jina la aliyekuwa Rais wa Zambia Kenneth Kaunda huvaliwa na Watu mbalimbali wakiwemo Viongozi na Wanasiasa na hata Rais wa Kenya William Ruto mara nyingi huvaa Kaunda suti kwenye hafla mbalimbali.
Spika Wetangula amesema mavazi sahihi Bungeni kwa Wanaume ni koti lenye collar, tai, shati lenye mikono mirefu, suruali ndefu, soksi, viatu, au uniform/sare maalum kwa watoa huduma na kwa Wanawake mavazi rasmi au nadhifu yenye heshima huku sketi na nguo zote zikitakiwa kuwa chini ya urefu wa goti, pia blauzi zisizo na mikono haziruhusiwi.
Spika wa Bunge Wetangula amekiri kwamba suti hizi zilivumiliwa hapo awali lakini sasa ni wakati wa kukomesha vazi hilo, kupigwa marufuku kwa suti hiyo kumezua hisia tofauti kwenye mitandao ya kijamii huku wengine wakishangaa ni kwa nini “vazi la Kiafrika” limepigwa marufuku na Bunge la Afrika, huku wengine wakiunga mkono, baadhi pia wamekejeli marufuku hiyo wakisema suti ya Kaunda sasa itakuwa ya Rais Ruto pekee.