Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 37, anayejulikana kwa jina la Lin, amekamatwa baada ya kushambulia watu 18 kwa kisu huko Jijini Shanghai, China, na kuua wa 3 na wengine 15 kuwajeruhi kutokana na ilivyodaiwa kuwa Mtu huyo alitekeleza shambulio hilo kutoa hasira zake.
Inaelezwa Shambulio hilo la kutisha lilitokea usiku kwenye Maduka ya shopping mall ya Walmart iliyopo maeneo ya Songjiang, eneo lenye msongamano mkubwa kusini magharibi mwa jiji la Shanghai, ambalo pia lina vyuo vikuu kadhaa. Watu watatu walikimbizwa hospitalini, kabla ya kufariki kutokana na majeraha waliyopata, huku hali za wahanga wengine 15 waliojeruhiwa haziripotiwi kuwa hatarishi kwa maisha.
Aidha, Polisi wamesema Lin alifika Jijini kutuliza hasira zake zinazotokana na mgogoro wa kifedha uliomkumba, Shahidi mmoja alieleza tukio hilo kuwa la kutisha, akisema hakuweza kuelewa kilichokuwa kikiendelea hadi alipoona watu wakikimbia kwa hofu na damu ikimwagika kwenye sakafu.
Inaripotiwa kuwa Matukio ya mashambulizi ya visu yameongezeka nchini China licha ya marufuku ya matumizi ya silaha, na yamekuwa chanzo cha hofu kwa wananchi.
Hata hivyo tukio hili limezua Mjadala kwenye mitandao ya kijamii nchini China, huku kukiwa na kumbukumbu za mashambulizi mengine kama haya, ikiwa ni pamoja na kifo cha mwanafunzi wa Kijapani mwezi uliopita.