Katika ripoti ya Jumanne, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilisema asilimia 50 ya watoto wa Somalia wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na utapiamlo unaotishia maisha.
Kati ya watoto wenye umri wa miezi 6 – 23, ni 1 tu kati ya 5 wanaolishwa mayai, samaki, kuku au nyama, na wawili kati ya watatu hawatumii mboga au matunda.
UNICEF inasema itashirikiana na serikali pamoja na washirika wengine ili kuboresha mfumo wa chakula kwa watoto wadogo na kuwezesha familia kupata aina mbalimbali za vyakula vinavyopatikana nchini Somalia hasa samaki, nyama, matunda na mbogamboga.
Takriban watu milioni 4 wanakabiliwa na mzozo au uhaba wa chakula wa dharura na watoto milioni 1.7 wanakabiliwa na utapiamlo nchini Somalia, wakiwemo 430,000 ambao wana uwezekano wa kuwa na utapiamlo mbaya mwaka 2024.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ilisema ufadhili wa dola bilioni 1.6 unahitajika kwa Mpango wa Mwitikio wa Kibinadamu wa 2024 (HNRP) nchini Somalia lakini ni dola milioni 507 pekee ndizo zimepokelewa kufikia Agosti Pili mwaka huu.