Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ameruhusu kupandishwa vyeo Maafisa, Wakaguzi na Askari 34,106, wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara yake kwa mujibu wa taratibu na sheria.
Akizungumza na Waandshi wa Habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, jijini Dodoma, leo, Simbachawene alisema idadi hiyo ya waliopandishwa vyeo ni kubwa na haijawahi kutokea katika historia ya Wizara hiyo ambayo inaongoza vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo ni Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji.
“Katika kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tayari Wizara yetu imewapandisha vyeo Maafisa, Wakaguzi na Askari wa ngazi mbalimbali 34,106 waliostahili kupandishwa vyeo katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021,” Simbachawene.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi limewapandisha vyeo jumla ya Maafisa, Wakaguzi na Askari 26,464, Jeshi la Magereza, limewapandisha vyeo jumla ya Maafisa, Wakaguzi na Askari 6,310, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 149, na Idara ya Uhamiaji, imewapandisha vyeo 1,183 ambapo kwa jumla ya vyombo vyote inafikisha idadi ya waliopandishwa vyeo kuwa 34, 106.
Aidha, Waziri Simbachawene amesema Rais Samia ametoa fedha kwa ajili kwenda kwenye mafunzo mbalimbali na kuanzia sasa matangazo yatakua yakitolewa kwa kada tofauti kwenda kwenye vyeo, na mafunzo hayo yatafanyika kwa miezi sita na miezi mitatu.
Waziri Simbachawene aliwapongeza Maafisa, Wakaguzi na Askari wote waliopandishwa vyeo na aliwataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na nidhamu kwa kufuata sheria za kazi na kuepuka vitendo vya rushwa kwa maendeleo ya Taifa.