Jeshi la Polisi Kigoma wakishirikiana na Askari wa JWTZ wamewaua Majambazi wawili huku Jambazi mmoja kutoweka kusikojulikana baada ya majibizano ya Risasi wakati Majambazi hao walipovamia Soko la Kijiji cha Bukirilo lililopo Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma ACP Menrad Sindano amesema ilikua ni usiku wa tarehe 21 July majira ya saa mbili ambapo Majambazi hao walifyatua Risasi hewani kuwatisha Wafanyabiashara na Wananchi kisha kufanikiwa kuiba vitu mbalimbali ikiwemo Vitenge, Pesa pamoja na Simu.
“Askari waliokua doria na askari wa JWTZ detach ya bukirilo walifika katika eneo hilo na kufanikiwa kuwajeruhi majambazi wawili kwa risasi ambapo walifariki dunia wakiwa njiani kupelekwa hosptali huku mmoja akikimbia”–ACP Menrad Sindano
Polisi wamesema baada ya kufanya ukaguzi wa eneo la tukio walifanikiwa kukamata silaha moja aina ya AK.47 yanye namba UG 2386 1998 na Magazine mbili,moja ikiwa na risasi 15 nyingine ikiwa tupu na kuokotwa maganda matatu ya risasi.
Aidha katika upekuzi wa miili ya marehemu hao zimepatikana simu tisa zilizoporwa kwenye duka na pesa taslim Tsh.82,000/= na vitambulisho vyao na vinaonyesha wanatoka nchi jirani.