Askari wanyamapori vijijini (VGS) watapatiwa miradi midogo midogo ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Maliasili na utalii wa kuimarisha uchumi wa wananchi wanaozunguka kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba kupitia mradi wa Kuimarisha utalii kusini REGROW.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula akijibu swali la Mhe. Venant Daud Protas Mbunge wa Jimbo la Igalula ambaye alitaka kujua lini Serikali itapeleka Askari na kulipa fidia kwa Wananchi waliovamiwa na tembo kwenye makazi na mashambani katika Jimbo la Igalula.
Aidha Mhe. Kitandula amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuharakisha kuwasilisha maombi ya kifuta jasho na kifuta machozi kufuatia changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.
Pia Mhe. Kitandula alisema kuwa serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa wananchi wanaozunguka hifadhi za taifa na mapori ya akiba ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya.
Vilevile Mhe. Kitandula alisema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeweka Askari sita wakiwemo Askari wa Uhifadhi wawili na Askari wa vijiji (VGS) wanne katika kituo cha kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu cha Ndala kilichopo katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Aidha, askari hao wamepewa vitendea kazi ikiwemo pikipiki mbili na silaha ambavyo vinawawezesha kudhibiti wanyamapori hao popote wanapoonekana ikiwemo Jimbo la Igalula.
Mheshimiwa Kitandula akijibu Swali la Mhe. Oliver Daniel Semuguruka Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera aliyataka kujua lini Serikali itaona umuhimu wa kukitangaza vya kutosha Kivutio cha Maporomoko ya Maji Rusumo ili kuchangia Pato la Taifa.
Mhe. Kitandula akijibu swali hilo amewataka wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuendelea kuibua vivutio vya utalii vinavyopatikana katika maeneo yao ikiwemo halmashauri ya Ngara.