Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema vifungashio vinavyotokana na malighafi ya plastiki na ambavyo havina nembo ya Shirika la Viwango (TBS), haviruhusiwi kutumika.
Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Nancy Nyenga, amesema kwamba, kwa kiwanda kitakacho zalisha vifungashio hivyo, kitatozwa faini ya Sh. milioni 20 na isiyozidi Sh. bilioni moja au kifungo cha miaka miwili jela au adhabu zote kwa pamoja
Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa NEMC, vifungashio vinavyolengwa ni pamoja na vinavyotumika kufungasha ubuyu, barafu na vyote vya plastiki visivyokuwa na nembo ya TBS.
Akizungumzia marufuku hiyo, amesema vifungashio vyote vya plastiki visivyokuwa na nembo ya TBS, havitaruhusiwakuanzia Januari Mosi mwaka huu, yaani leo, kwa kuwa serikali imeshapiga marufuku na kuelekeza vifungashiovinavyoruhusiwa.
“Sheria ya mazingira ya kuzuia mifuko ya plastiki ilianza kutumika juni mwaka jana na serikali kupitia NEMC ilitoa maelekezo ya vifungashio vinavyoruhusiwa kuwa ni pamoja na vile vyenye nembo ya TBS kutoka viwandani ” Nyenga.