Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso (Mb) amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa katika kuhakikisha majengo ya Wizara mbalimbali katika mji wa serikali Mtumba, ikiwa ni pamoja na jengo la Wizara ya Maji katika kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira mazuri.
Amesema hayo alipotembelea na kukagua jengo la Wizara ya Maji jijini Dodoma katika Mji wa Serikali Mtumba ambalo limekamilika kwa asilimia 99.
Jengo hilo lina ghorofa sita, vyumba 281 na linauwezo wa kuchukua watumishi wasiopungua 455 .
Pia jengo hili lina kumbi 12 za mikutano ukiwemo ukumbi mkubwa wenye uwezo wa kuhudumia watu 155.
“Sasa hatuna kisingizio, tumepata ofisi nzuri za kisasa. Hatuna cha kumlipa Mhe. Rais isipokuwa utendaji mzuri ambao utawezesha matokeo chanya.” Aweso amesema na kusisitiza ushirikiano katika utendaji kazi ili kuharakisha matokeo tarajiwa.
Amewataka watendaji wa wizara kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ili kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila Mtanzania kama Serikali ilivyopanga kuwahudumia wananchi katika suala la huduma ya maji.
Pamoja na hayo amemshukuru Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb na ofisi yake kwa kazi kubwa ya uratibu wa ujenzi wa mji wa serikali ambapo kazi katika maeneo mbalimbali inaendelea kwa kasi.