Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amesema muungano wao wa Azimio la Umoja-One Kenya, unaendelea kukusanya ushahidi ambao itauwasilisha katika mahakama ya ICC, kuonesha namna serikali inatumia vyombo vya usalama kunyanyasa na kuua raia wanaoshiriki maandamano ya amani.
Aidha Odinga, amesema bado yuko tayari kukutana na rais William Ruto kuangalia namna atashughulikia madai yao, hata hivyo akimtuhumu kukaidi wito wa viongozi wa ukanda wanaojaribu kuwapatanisha.
Sasa naweza kusema hapa wazi kwamba rais wa Tanzania alikuja hapa wiki mbili zilizopita, baada ya kualikwa na rais Ruto ili kujaribu kutusaidia katika mazungumzo lakini alilazimishwa kusubiri kwa muda mrefu na baadaye akaamua kuondoka.
Odinga ameyasema haya hivi leo alipozungumza na vyombo vya habari vya kimataifa jijini Nairobi, na hii ni baada ya ukimya wa karibu wiki moja tangu maandamano ya wiki iliyopita, maandamano ya kulalamikia gharama ya juu ya maisha.
Tangu mwezi Machi mwaka huu, Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, umeandaa mikutano tisa ya maandamano dhidi ya serikali ya rais Ruto, katika maandamano ambayo waandamanaji na vikosi vya usalama wamekuwa wakikabiliana.
chanzo:RFI